Friday, August 08, 2014

WAKULIMA WATAKIWA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO



WAKULIMA WATAKIWA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO
Na Woinde Shizza,Arusha

Wakulima wametakiwa kutumia fursa ya kuongeza thamani mazao yao ili waweze kunufaika zaidi kiuchumi kuliko kuuza mazao yao yakiwa ghafi kwani watakuwa wanayonywa na kuzidi kuwa masikini.

Wito huo umetolewa jana na Ofisa masoko wa shirika la Farm Africa, Rahel Pazzia, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwenye maonyesho ya wakulima nane nane, kanda ya kanda ya kaskazini yanayoendelea jijini Arusha.  

Alisema kupitia Farm Africa wakulima wengi wa ufuta wa mkoa huo wamenufaika kiuchumi kutokana na kuongeza thamani mazao yao na kutouza yakiwa ghafi hivyo kujiongezea kipato zaidi kinachowaletea maendeleo.

"Farm Africa inawataka wakulima nchini waje wajifunze kupitia wakulima wetu wa ufuta, hivi sasa wananufaika zaidi kiuchumi kwani badala ya kuuza ufuta, wanaongeza thamani kwa kutengeneza mafuta, kashata, sabuni na kinywaji," alisema Pazzia.   

Alisema wakulima sita wamefika kwa ajili ya kuonyeshaji mazao ya ufuta na misitu na wakulima 45 wamekuja kujifunza kwa ajili ya kuongeza elimu zaidi na pia kutoa elimu kwa wakulima wengine ili wajifunze kupitia wao.

Naye, Ofisa miradi wa misitu na masoko wa shirika hilo, Hakam Mohamed alisema wanavijiji 33 wa wilaya ya Mbulu na Babati mkoani Manyara, wananufaika kupitia msitu Nou na lengo lao ni kuijengea jamii uwezo zaidi wa kiuchumi.

Mohamed alisema ili kuhakikisha jamii haiharibu msitu huo kwa kuutumia kwa matumizi yasiyo ya mazuri wamebuni miradi ya kurina asali, miche ya miti, kulima uyoga na ususi wa vikapu, ambayo imewanufaisha wote wanayozunguka Nou.

"Tumewawezesha wawe na vicoba, wapate mikopo ili waweze kuibua miradi ambayo itawanyanyua kiuchumi na kutokuwa na wazo baya la kuharibu msitu wa Nou ikiwemo kukata miti kwa ajili ya kupata mbao," alisema Mohamed.

Kwa upande wake, mkulima wa ufuta wa kijiji cha Ngolei, Costantine Martin alisema kupitia ufuta amenufaika kiuchumi kuliko kulima mahindi kwani gunia moja la kilo 85 anauza sh215,000 huku gunia moja la mahindi likiuzwa sh30,000.

Naye, mrina asali wa kijiji cha Boboa wilayani Mbulu, Philemon Lawrence alisema kupitia shirika la Farm Africa, wameweza kujinufaisha kiuchumi kwa kuwezeshwa kupitia miradi mbalimbali ikiwemo kupatiwa mizinga ya nyuki.
 Ofisa masoko wa shirika la Farm Africa, Rahel Pazzia (kulia) akiwa na baadhi ya wakulima wa ufuta wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara jana, katika banda la Farm Afrika kwenye maonyesho ya wakulima nane nane kanda ya kaskazini, yanayofanyika viwanja vya Themi jijijni Arusha.

Watanzania wenye asili ya bara Asia wakipewa maelezo ya ubora wa mafuta ya ufuta kwenye banda la shirika la Farm Africa, katika maonyesho ya wakulima nane nane kanda ya kaskazini, yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi jijini Arusha.