Wednesday, August 06, 2014

Mnaoishi Nje ya nchi Acheni Kupoteza Muda Kwenye Blogs na Kulaumu Wengine Kuhusu Uraia Pacha..Leteni Hoja



Mnaoishi Nje ya nchi Acheni Kupoteza Muda Kwenye Blogs na Kulaumu Wengine Kuhusu Uraia Pacha..Leteni Hoja
RAIS Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania waishio nje ya nchi na wanaotaka kuona Tanzania inakubali kuanzisha mfumo wa uraia pacha, kutumia muda wao kujenga hoja za jambo hilo badala ya kupoteza muda kwenye mijadala ya 'blogu' na kulaumu watu wengine.

Pia, aliwataka watanzania hao kusema ili wasikike, kwa sababu kimsingi hoja ya uraia pacha haina nguvu miongoni mwa Watanzania wanaoishi Tanzania, bali inatokana zaidi na msukumo wa Watanzania wanaoishi nje, ambao kwa bahati mbaya hawafanyi jitihada za kutosha kutetea hoja yao.

Aliwaambia watanzania hao, kuacha kupoteza muda kujadili mambo yasiyokuwa na maana, badala yake kuelekeza nguvu zao katika kujenga hoja yenye nguvu zaidi ya uraia pacha, jambo ambalo ni moja ya mambo yatakayojadiliwa katika mchakato wa Katiba mpya.

"Ushauri wangu ni kwamba tumieni muda wetu kusaidia kusukuma hoja yenu hii muhimu ambayo kama mnavyojua imeingizwa katika rasimu kwa mapendekezo ya CCM kwa sababu suala hilo halikuwemo katika rasimu ya kwanza," alisema.

Rais Kikwete, ameyasema hayo Agosti 2 mwaka huu, wakati alipokutana na Watanzania wanaoishi Marekani,  hasa katika maeneo ya Jiji la Washington D.C na majimbo ya Virginia, Maryland, New York na hata California katika mkutano uliyofanyika hoteli ya Marriot Washington mjini Washington D.C.

Rais yuko katika ziara ya siku tisa nchini Marekani, ambako miongoni mwa mambo mengine atahudhuria mkutano wa kwanza wa Marekani na Afrika ambao shughuli zake zimeanza jana.