Thursday, July 03, 2014

MALKIA WA SWAZILAND AICHANGIA SHULE YA SEKONDARI YA WAMA-NAKAYAMA ZAIDI YA MILIONI TANO


MALKIA WA SWAZILAND AICHANGIA SHULE YA SEKONDARI YA WAMA-NAKAYAMA ZAIDI YA MILIONI TANO
IMG_5688 Mwanafunzi Elizabeth Kipoto anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya wasichana ya Wamanakayama akiwaonyesha wageni jaribio la kujua kama kuna protini kwenye vyakula katika maabala ya Biologia shuleni hapo tarehe 2.7.2014.
PICHA NA JOHN LUKUWI
Na Anna Nkinda- Maelezo
 Mke wa Mfalme wa Swaziland  Malkia Nomsa Matsebula ameipatia  shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani zaidi ya  shilingi milioni tano ili ziweze kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo katika mahitaji yao ya kila siku.Malkia Matsebula ambaye ni Mke wa Mfalme Muswati  alitoa fedha hizo jana wakati alipoitembelea shule hiyo ambayo ni ya bweni  inayopokea Watoto yatima na wanaotoka  kwenye familia maskini kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Akiongea na wanafunzi hao Malkia Matsebula aliwataka wanafunzi hao kutumia nafasi hiyo kusoma kwa bidii kwani  msichana ni mtu anayeyashika maisha yake ya baadaye katika mikono yake kwa kujenga nyumba ya upendo, kufanya  kazi zake vizuri kwa kuona jamii yake inakuwa.
Aliwataka kusoma masomo ya aina mbalimbali ili hapo baadaye waweze kuwa   na taaluma mbalimbali zikiwemo za ujenzi, injinia ,sheria, uhasibu kwani elimu haitoki katika mti bali ni mpangilio ambao  mwanafunzi anajipangia. 
"Kumbukeni kuwa Elimu haipatikani shuleni peke yake bali hata katika jamii inayowazunguka kwani kwenda shule siyo kama umeelimika bali unatakiwa kuvifanyia kazi vile ambavyo  umejifunza, wanawake onyesheni  elimu yenu kwa  vitendo ili jamii inufaike na elimu hiyo.
Wanawake ni watu wanaopenda jamii ingawa  wanakutana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, kuacha shule, unyanyasaji wa kijinsia kwani bila ya wao hakuna maendeleo  katika nchi , nyinyi tumieni nafasi hii kusoma kwa bidii ili hapo baadaye muweze kuzitatua changamoto hizo", Malkia Matsebula alisema.
Aliwasihi wanafunzi hao kujenga tabia ya kujiheshimu katika maisha yao ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuongea na kuvaa mavazi ya heshima na kuheshimu wengine kwani  Elimu inakuja kwa kujiheshimu. 
Aidha Malkia Matsebula aliwaomba wadau wengine wa maendeleo kumuunga mkono Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu jambo ambalo litasaidia kupatikana kwa viongozi na wanawake wengi wasomi hapo baadaye. 
Kwa upande wa walimu aliwataka kuwafundisha wanafunzi hao Historia ya nchi yao na Bara la Afrika kwa ujumla ili wajue ni wapi walikotoa na viongozi wao walikuwa wanafanya mambo gani. Kwa kufanya hivyo wataweza kuilinda na kuitetea nchi na bara lao.
Naye Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alimshukuru Malkia Matsebula kwa kutembelea shule hiyo na kusema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa kama mtoto wa kike atapata  elimu ya kutosha tatizo la ndoa za utotoni, vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vitapungua.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo inayoendesha shule hiyo; alisema walichagua elimu kwa mtoto wa kike kuwa moja ya kazi zinazofanywa na yake kwa  kuamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha ambayo mwanamke alikuwa ameikosa kwa muda mrefu.
"Taasisi ya WAMA iliamua kujenga shule hii ili kuweza kutoa elimu kwa watoto wa kike ambayo ni yatima na  wanatoka katika mazingira hatarishi kwani  watoto hawa walikosa nafasi ya kusoma ukilinganisha na watoto wengine", alisema Mama Kikwete.
Shule hiyo ya kidato cha kwanza hadi cha nne ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 83 hadi sasa idadi ya wanafunzi imekuwa na kufikia 336 na katikati ya mwezi huu inampango wa kuanzisha kidato cha tano na cha sita.
Licha ya kutembelea shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama Malkia Matsebula aliitembelea Taasisi ya WAMA iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo pia alishiriki chakula cha jioni kilichoandaliwa na mwenyeji wake Mama Salma Kikwete.