Na Lucas Mboje
Watanzania wametakiwa kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa na Jeshi la Magereza hapa nchini zikiwemo Samani za ndani na Ofisi.
Mwito huo umetolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja wakati akiongea na Waandishi wa Habari mara tu baada ya kutanganzwa rasmi Jeshi la Magereza kuwa Mshindi wa kwanza kwa upande wa utengenezaji wa bidhaa za Samani za ndani katika Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika uwanja wa Mwalimu Nyerere uliopo Barabara ya Kilwa Wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam.
"Kuna Maboresho makubwa sana juu ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na Jeshi la Magereza na hiyo ndo imepelekea Jeshi la Magereza kuibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa utengenezaji bora wa Samani za ndani katika Maonesho haya ya 38 ya Biashara yanayoendelea". Alisema Kamanda Jenerali Minja.
Aliwashukru Wananchi mbalimbali kwa kuzipenda bidhaa zilizopo katika Banda la Jeshi la Magereza na kuwaomba Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa DSM kutembelea Banda la Jeshi la Magereza ili waweze kujipatia bidhaa bora pia kuona na kujifunza.
Pia Kamishna Jenerali Minja amewapongeza Maofisa na Askari wa Jeshi la Magereza wanaoshiriki katika Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa kwa kufanikisha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa utengenezaji wa Samani za ndani katika Maonesho hayo yanayoendelea, Jijini Dar es Salaam.