Saturday, July 05, 2014

Balozi seif ali Iddi atembelea Kijiji cha Kilombero




Balozi seif ali Iddi atembelea Kijiji cha Kilombero
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Nd. Hassan Ali Hassan alisema shirika lake linakusudia kutumia rasilmali ilizonazo katika kuhakikisha huduma za umeme zinapatikana kwenye kisima cha maji cha Kijiji cha Kilombero ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma za maji safi  kwa Wananchi wa Kijiji hicho. 
Alisema kazi hiyo itakayoanza wakati wowote kuanzia sasa inatarajiwa kukamilika sambamba na ulazwaji wa mabomba ya maji utakaofanya na wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kutoka kwenye kisima hicho hadi maeneo ya wakaazi wa Kijiji hicho. 
Nd. Hassan Ali Hassan alitoa kauli hiyo mara baada ya kupokea hundi ya shilingi Milioni 14,000,000/- zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kupitia mfuko wa Jimbo ili kuanza kazi za kukipatia umeme kisima hicho kilichopo ndani ya shamba la ASP mashariki mwa Kijiji cha Kilombero. Alisema licha ya gharama halisi zinazohitajika katika mradi huo wa umeme zinayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi Milioni 60,000,000/- ikijumuisha nguzo, waya pamoja na transfoma lakini shirika litajitahidi katika kuona mradi huo unafanikiwa ili umeme upatikane katika kisima hicho. 
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu alisema kisima hicho tayari kimeshakamilika kwa muda mrefu sasa, lakini kilichobakia ni kusambazwa kwa mabomba kazi itakayochukuwa muda kidogo. 
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho cha Kilombero Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza wanakiji hao kwa ustahamilivu wao mkubwa wa kukosa huduma za maji safi na salama kwa muda mrefu. Zaidi ya shilingi Milioni 20,000,000/- zilizotolewa na Mbunge wa jimbo la Kitope Balozi Seif zimetumika kugharamia ujenzi wa kibanda cha kisima hicho kilichochimbwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu akitoa ufafanuzi kwa wananachi wa Kijiji cha Kilombero Wilaya ya Kaskazini " B " juu ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kisima cha maji safi na salama cha kijiji hicho.
Ufafanuzi huo aliutoa wakati wa hafla fupi ya Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kukabidhi  hundi  ya shilingi milioni 14,000,000/- kwa ajili ya uwekwaji wa huduma za umeme katika Kisima hicho.
 Mbunge wa Jimbo la Kitop[e ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwapongeza wananchi wa Kijiji cha kirombero kwa ustahamilivu wao wa muda mrefu kutokana na ukosefu wa huduma ya maji safi yanayotarajiwa kupatikana muda si mrefu kijijini hapo.
Balozi Seif akimkabidhi Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Nd. Hassan Ali Hassan Hundi ya shilingi Milioni 14,000,000,/- kwa ajili ya uwekwaji wa huduma za umeme kwenye kisima cha maji cha kijiji cha Kilombero.
Aliyepo kati kati yao ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B " Nd. Khamis Jabir Makame. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.