Saturday, June 14, 2014

Balozi Seif akabidhi kadi kwa wanachama wapya 15 wa CCM Mkoa wa Magharibi,Zanzibar




Balozi Seif akabidhi kadi kwa wanachama wapya 15 wa CCM Mkoa wa Magharibi,Zanzibar
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif akimkabidhi kadi mwanachama mpya wa CCM Shina nambari 23 la Tawi la CCM Fuoni Bibi Faiza Chande Ameir.Kushoto ya Balozi ni Mwenyekiti wa Shina Nambari 23 la Tawi la CCM Fuoni Nd. Daudi Khamis, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Magharibi Nd. Yussuf Mohd Yussuf na Katibu wa CCM Mkoa huo Aziza Ramadhan Mapuri.
Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe Ndugu Khamis Juma Msonge akimkaguza Mjumbe wa Kamat Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi kuangalia jengo la Ofisi ya Jimbo hilo ambayo iko katika hatua za mwisho za ujenzi wake. Balozi Seif akiwa mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama alikuwa katika ziara ya kichama ndani ya Wilaya ya Dimani. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mafanikio ya Uongozi ndani ya Mashina ya Chama cha Mapinduzi ni nguzo pekee inayosaidia uimarishaji wa chama hicho katika ngazi zote.

Alisema hayo wakati akizungumza na wanachama wa Shina nambari 23 la CCM Tawi la Fuoni baada ya kugawa kadi kwa wanachama wapya 15 wa CCM wa Shina hilo akiwa katika ziara ya kutembelea Wilaya ya Dimani Kichama akiwa mlezi wa Mkoa wa Magharibi.

Balozi Seif alisema kwa kuwa chama imara ni kile kinachoungwa mkono na watu walio wengi popote pale aliwapongeza Vijana hao wa shina nambari 23 kwa uamuzi wao wa busara wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi.

Alisema nguvu ya Chama ni Vijana ambao pia ni tegemeo kwa Taifa. Hivyo aliwataka waendelee kushikamana pamoja ili kuongeza uzalendo wao katika kulitumikia Taifa lao.

Katika kuunga mkono juhudi za wanachama hao wa CCM Shina nambari 23 Fuoni Balozi Seif aliahidi kuwapatia seti ya TV Pamoja na King'amuzi chake ili wapate fursa ya kupata habari, burdani pamoja na kuona mashindano ya kombe la dunia yanayoendelea hivi sasa Nchini Brazil.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa akiwa pia ni mlezi wa Mkoa wa Magharibi aliitembelea Ofisi ya CCM Jimbo la Mwanakwerekwe kukagua hatua iliyofikia ya ujenzi jengo lao na kuwapongeza wana CCM hao kwa uamuzi wao wa kujenga Ofisi mpya ya Jimbo hilo inayokwenda na wakati.