Jeshi la polisi mkoani Njombe limeamua kuchukua uamuzi mgumu wa kuwafukuza kazi askari polisi wake watatu kwa makosa mbalimbali waliyoyafanya ikiwemo vitendo vibaya kinyume na sheria za jeshi hilo
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa mtandao huu na kamanda wa polisi mkoa wa Njombe SACP Fulgence Ngonyani (pichani) askari hao waliofukuzwa kazi ni EX.G. 3172 PC Ramadhani Iddi Saidi, EX.G. 9693 PC Emmanuel Morson Lyimo pamoja na EX.G. PC Miraji Jumanne Mtea
Kamanda Ngonyani amesema Jeshi la polisi limeamua kutoa adhabu hiyo kali kutokana na vitendo mbalimbali vya utovu wa nidhamu walivyovifanya ikiwemo tukio la hivi karibuni la kupigana hadharani Septemba 2 mwaka huu Mjini Njombe
Amesema wanategemea adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa askari wengine wenye tabia kama hiyo kwani jeshi halitawavumilia askari wake ambao wanakwenda kinyume cha sheria
Katika hatua nyingine Kamanda Ngonyani amewataka wananchi kuwa makini na askari hao waliofukuzwa kazi huku akisisitiza wananchi kutambua kuwa askari hao si watumishi tena kuanzia Oktoba 24, mwaka huu
Na Edwin Moshi