Saturday, February 23, 2013

Hii ndio Miji yenye gharama kubwa zaidi duniani


 
LONDON, Uingereza
MIJI ya Sydney na Melbourne ni miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuwa na gharama kubwa zaidi za maisha duniani.
Miji hiyo ambayo iko nchini Australia, imeingia katika nafasi ya tano bora.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kitengo cha Kiintelijensia cha Uchumi Duniani (EIU), gharama za maisha katika miji hiyo imezidi hata miji ya Ulaya na Marekani.
Bara la Asia na Australia lina miji 11 kati ya 20 iliyotajwa kuwa na gharama za juu za maisha duniani, huku miji minane ikitoka Ulaya na mmoja ukitoka America ya Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kitengo hicho, licha ya bara la Amerika ya Kaskazini kuwa na nchi maarufu na zenye uchumi wa juu, hakuna hata mji mmoja ulioweza kuingia kwenye 20 bora.
Katika utafiti uliofanyika miaka 10 iliyopita kulikuwako na  miji sita kutoka barani Asia, 10 kutoka Ulaya na minne kutoka Marekani katika 20 bora kwenye orodha ya miji 131 yenye gharama za juu kwenye nchi 93 duniani.
Katika utafiti  uliotolewa mwaka huu, Jiji la Tokyo limeshika nafasi ya kwanza likiliweka pembeni Jiji la Zurich ambalo lilikuwa kwenye nafasi hiyo na kuporomoka hadi kufikia nafasi ya saba.
Hii ni kutokana na sera za udhibiti wa mapato ya ndani ya nchi ya Uswiz kushuka.
Mji wa Osaka nchini Japan unashikilia nafasi ya pili katika orodha hiyo.
Jon Copestake, mhariri wa jarida la EIU alisema moja kati ya mabadiliko yaliyojitokeza ilikuwa ni kupanda kwa gharama nchini Australia, kulikouweka Mji wa Sydney kushika nafasi ya tatu huku Melbourne ikishika nafasi ya tano. Mji wa Oslo wa Norway ukishika nafasi ya nne. "Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, miji ya Australia haikuweza kuingia hata kwenye hamsini bora. Sijawahi kuona upandaji huu wa ghafla," Copestake aliliambia Reuters.
"Lakini hii inatokana na kukua kwa uchumi kunakoendana na mfumuko wa bei pamoja na  kuimarika kwa Dola ya Australia dhidi ya Dola ya Marekani. Wageni wanaofika hapo huona kuna tofauti kubwa ya kimaisha huku wenyeji wakizoea maisha ya juu.
Kupanda kwa gharama barani Asia
Utafiti huo ulifanyika kwa kuangalia gharama za zaidi ya bidhaa 160 ukilenga kwenye vyakula, mavazi, huduma za nyumbani, usafiri na vitu vidogovidogo.
Copestake haikushangaza sana kwa Mji wa Tokyo kurejea kwenye miji ya inayoongoza, hii ni kutokana na kukua kwa uchumi wa Japan jambo linalosababisha kuongezeka kwa gharama za mahitaji muhimu kama vile mapango ya nyumba, mishahara na hata bei za nishati ya mafuta.
Tangu mwaka 1992 Tokyo imekuwa kwenye sita bora huku miji ya  Zurich, Paris na Oslo ikidaiwa kushika nafasi ya kwanza.
Miji mingine iliyoingia kwenye 10 bora kwa mwaka 2013 ni Singapore, Zurich, Paris,Caracas na Geneva.
Akizungumzia kuhusu nchi za Ulaya, Copestake alisema woga wa kushuka kwa uchumi wao na kuimarika kwa Euro kumechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa gharama za maisha kwa miji ya bara hilo, huku kwa Mji wa Carcas kumetokana na kukua kwa udhibiti wa viwango vya ubadilishaji wa fedha.