Friday, September 21, 2012

TAARIFA YA MWELEKEO WA AJALI ZA BARABARANI NCHINI ILIYOSOMWA NA KAMANDA WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI (T) SACP. M.R.A MPINGA KATIKA MKUTANO MKUU WA BARAZA LA TAIFA LA USALAMA BARABARANI MKOANI IRINGA TAREHE 20/09/2012


 Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani hilo na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mohamed Mpinga, akitoa taarifa ya Usalama barabarani kwa mwaka uliopita mbele ya wajumbe wa Baraza hilo.
---
TAARIFA YA MWELEKEO WA AJALI ZA BARABARANI NCHINI ILIYOSOMWA NA KAMANDA WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI (T) SACP. M.R.A MPINGA KATIKA MKUTANO MKUU WA BARAZA LA TAIFA LA USALAMA BARABARANI MKOANI IRINGA TAREHE 20/09/2012

Ajali za barabarani ni tatizo ambalo linaendelea kuikumba nchi yetu. Jambo ambalo limeendelea kupoteza maisha ya watanzania na wengine kupata vilema vya maisha kila kukicha. Tatizo hili halijafumbiwa macho kwani kumekuwa na jitihada mbalimbali za serikali kupitia Jeshi la Polisi pamoja na wadau mbalimbali za kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hili. Inafahamika wazi kuwa madhara yatokanayo na ajali ni vifo, vilema vya kudumu, na upotevu wa mali. Vifo na vilema vimepelekea upotevu wa nguvu kazi, umaskini na yatima kwa familia za waathirika. Aidha ajali zimekuwa zikiigharimu serikali fedha nyingi kwa kugharamia matibabu ya waathirika wa ajali na kuathiri uchumi wa taifa. 

                TAKWIMU ZA AJALI ZA BARABARANI T(BARA)MWAKA 2005-2011
 
MWAKA    AJALI    VIFO    MAJERUHI
2005    16,388             2,430           16,286
2006    17,677             2,884           15,676
2007    17,753                2,594        16,308
2008    20,615               2,905        17,861
2009    22,739              3,223         19,263
2010    24,665               3,582        20,656
2011    23,986                3,981      20,802



Kwa ulinganisho wa ajali za barabarani kwa mwaka 2010 na 2011,  ajali zilipungua kwa 679 sawa na 3%, vifo vimeongezeka kwa 399 sawa na 11%, na majeruhi 146 sawa na ongezeko la 0.7%. 

            TAKWIMU ZA AJALI ZA BARABARNI (T) BARA JAN-JUNE 2011/2012
2011 JAN-JUNE    2012 JAN-JUNE
AJALI    VIFO    MAJERUHI    AJALI    VIFO    MAJERUHI
12,124    1,764       10,122             11,163    1,808       9,155


Pia kwa Katika miezi 6 ya mwaka 2012 (jan-june) kumekuwa na ajali 11,163 ikiwa ni pungufu la ajali 961 kwa kulinganisha na ajali 12,124 za mwaka 2011 (Jan-June).
Aidha kwa mwaka 2012 (Jan-June) kuna  vifo 1,808 ikiwa ni ongezeko la vifo 44 kwa kulinganisha na vifo 1,764  vilivyotokea mwaka 2011 (Jan-June).
Vilevile kwa mwaka 2012 (Jan-June) kuna majeruhi 9,155 ikiwa ni upungufu wa majeruhi 967 kwa kulinganisha na majeruhi 10,122 waliojeruhiwa mwaka 2011 (Jan-June).

AJALI ZA PIKIPIKI
Ajali za pikipiki nazo zimeendelea kuongezeka hapa nchini. Chanzo kikubwa cha ajali ni ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki na kukosa sifa ya kumiliki leseni ya udereva inayothibitisha kuhudhuria mafunzo katika chuo kinachotambulika na serikali  na kufuzu mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki.  Tatizo hili limesababisha wao kutozijua sheria na kanuni za Usalama Barabarani sambamba na kutozijua alama za barabarani, uendeshaji wa hatari kwa kupenyeza katikati ya magari na kuyapita (careless overtakings), mwendo kasi, kutovaa kofia ngumu, na upakiaji wa abiria zaidi ya mmoja (mshikaki). 

Vilevile ajali zitokanazo na waendesha pikipiki zimekuwa zikisababishwa na udhibiti hafifu wa uagizaji na uingizaji wa pikipiki hapa nchini kwa mamlaka zinazohusika (hakuna sera ya kudhibiti vyombo hivi) jambo ambalo limepelekea kuwa na wafanya biashara wengi wa pikipiki na wingi wa pikipiki unaosababisha kila mtu kuwa na uwezo wa kumiliki pikipiki hasa kwa vijana wasio na ajira na kuzitumia kibiashara baada ya serikali kuruhusu pikipiki kutumika kusafirisha abiria.

Miundo mbinu yetu haikidhi matumizi ya vyombo vya moto kwa nafasi. Hii inatokana na barabara nyingi za mjini kuwa nyembamba sana na kusababisha ajali za magari kugongana na pikipiki kutokea mara kwa mara na waathirika wakubwa wakiwa ni wapanda pikipiki
 
TAKWIMU ZA AJALI ZA PIKIPIKI (T) BARA KWA MWAKA 2007 HADI 2011
MWAKA    AJALI    VIFO    MAJERUHI
2007               1683        193        1423
2008             2036           309    1931
2009            3406    502    3478
2010    4363    683    4471
2011    5384    945    5506


Katika kipindi cha mwaka 2011 kulikuwa na ajali za pikipiki 5,384 kwa kulinganisha na ajali 4,363 zilizotokea mwaka 2010 sawa na ongezeko la 23%, vifo 945 kwa kulinganisha na vifo 683 sawa na ongezeko la 38%, na majeruhi 5,506 kwa kulinganisha na majeruhi 4,471 sawa na ongezeko la 23%.

            TAKWIMU ZA AJALI ZA PIKIPIKI (T) BARA  MWEZI JAN-JUNE 2011/2012
2011 JAN - JUNE                            2012 JAN- JUNE
 
AJALI    VIFO    MAJERUHI    AJALI    VIFO    MAJERUHI
2,856    396    2562    2641    487    2,706


Katika kipindi cha mwezi Jan-June 2012 kumekuwa na ajali za pikipiki 2,641 kwa kulinganisha na ajali 2,856 zilizotokea mwezi Jan-June 2011 sawa na pungufu la ajali 215, vifo 487 kwa kulinganisha na vifo 396 sawa na ongezeko la vifo 91, na majeruhi 2,706 kwa kulinganisha na majeruhi 2,562 sawa na ongezeko la majeruhi 144.

CHANGAMOTO KATIKA KUKABILIANA NA AJALI ZA BARABARANI
1.    Ukosefu wa elimu ya Usalama Barabarani kwa watumiaji wa barabara, na kwa baadhi yao wenye elimu kutokubali kuitumia elimu hiyo kutii sheria na kanuni za Usalama Barabarani.
2.    Ongezeko la idadi ya magari isiyoendana na miundo mbinu iliyopo.
3.    Uchache wa vitendea kazi usiokidhi mahitaji ya kazi za barabarani.
4.    Adhabu / faini kwa makosa ya Usalama Barabarani kuwa ndogo.
5.    Kukosekana kwa utashi kwa viongozi wa kisiasa kuzungumzia tatizo la ajali za barabarani.


MIKAKATI YA KUPUNGUZA AJALI ZA BARABARANI
i.    KUTEKELEZA KWA VITENDO MUONGO WA UMOJA WA MATAIFA WA USALAMA BARABARANI   (UN DECADE OF ACTION FOR ROAD SAFETY) 2011 – 2020.
Kikosi cha Usalama Barabarani kinashirikiana na Idara    mbalimbali kutekeleza mambo yaliyolengwa kusimamiwa kwa umakini ili kufikia lengo la kupunguza ajali, vifo na majeruhi kwa 50% ifikapo 2020. Miongoni mwa mambo yatakayosaidia kufikia malengo hayo ni kama ifuatavyo.

i. Menejimenti ya usalama barabarani (Road Safety Management),

ii. Barabara salama (Safer roads and Mobility),

iii. Magari salama (Safer vehicles),

iv. Watumiaji salama wa barabara (Safer Road users),

v. Kuimarisha huduma baada ya ajali au uokoaji (post crash response),

Tanzania ambayo pia ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa nayo ipo katika mchakato wa utekelezaji wa azimio hilo la Umoja wa Mataifa la kupunguza ajali za barabarani.


ii.    SMARTER TRAFFIC PROGRAMME.

Smarter Traffic ni mpango unaoelenga kuboresha mwenendo wa shughuli za usalama barabarani Tanzania. Mpango huu unatokana na utafiti uliofanywa na kampuni ya IBM-International Bussiness Machine toka Marekani. Katika utafiti huo ulibainisha maeneo saba ambayo yakifanyiwa kazi ipasavyo swala la ajali na kero za barabarani zitakwisha.
i).Elimu ya Usalama barabarani inahitajika kwa jamii yote Tanzania.
ii).Unahitajika usimamizi wa vyombo vya moto vikiwa barabarani.
iii).Kuwa na Kanuni za uagizaji wa vyombo vya moto vyenye usalama.
iv).Kushirikishwa kwa wadau mbalimbali kutaleta tija barabarani.
v).Kuwa na barabara salama zinazokidhi watumiaji wote wa barabara.
vi).Kuwa na vifaa vya mawasiliano kwa Jeshi la polisi na idara husika.
vii).Kusimamia sheria na kanuni zilizopo.

Kikosi cha Usalama barabarani kimeanza kuyafanyia kazi baadhi mambo hayo.

iii.    JUNIOR PATROL PROGRAMME
Tunaendelea kutoa mafunzo kwa watoto wa shule kuweza kujivusha wenyewe. Mpango wa kujivusha barabarani ulianza kwa shule za msingi 12 zilizopo mkoani Dar es Salaam na zimeongezeka na kufikia shule 22. Mikoa mingine iliyoanza kutekeleza mpango huu ni Arusha, Morogoro, Kagera Mbeya, Tabora, Shinyanga na Dodoma. Lengo la mpango huu ni kuwaepusha wanafunzi kugongwa na magari wakati wanavuka barabara na kuwajengea uwezo wa kujiamini wanapotumia barabara. Mpango huu ni endelevu. 

iv.    TRAFFIC WARDEN PROGRAMME.
Huu ni mpango wa kuwatumia wananchi katika kusimamia sheria za Usalama Barabarani. Lengo kubwa la kuanzisha mpango huu ni kuhamasisha wananchi washiriki katika kusimamia sheria za usalama barabarani. Kwa sasa kuna askari 40 wa manispaa ya Ilala ambao wamepata mafunzo ya Usalama Barabarani na watasaidia kutatua kero na makosa yanayofanywa na watumiaji wa barabara. Mpango huu ukifanikiwa kuleta ufanisi katika Manispaa ya Ilala tutaueneza nchi nzima.


v.     MPANGO MKAKATI WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI (STRATEGIC PLAN) 2011/2015 

Katika kuhakiksha Kikosi cha usalama barabarani kinatekeleza mipango yake kwa ufanisi, Inspekta Jenerali wa Polisi Afande Said Ally Mwema aliona ni vyema Kikosi hiki kuwa na Mpango Mkakati. Mnamo tarehe 23.03.2012 aliteua Kamati Maalum itakayohusika katika kuandaa Mkakati huo. Manamo tarehe 26.03.2012 Kamati hiyo ilianza kazi rasmi ya kutekeleza jukumu hilo. Katika kuhakikisha mpango unafanikiwa Kamati ilipitia wadau mbalimbali wa Usalama Barabarani ili kupata maoni yao. Wadau waliotembelewa ni NIT, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya DPP, TAMISEMI, TANROADS, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya, MOI, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, SUMATRA, Ofisi ya Kamishna wa BIMA na Taasisi ya Elimu Tanzania.

Maoni ya Wadau yalisaidia katika kuwa na mwelekeo mpana wa kuandaa mpango Mkakati mzuri. Mambo muhimu yaliyozingatiwa katika Mpango Mkakati huo ni haya yafuatayo:

1.    Elimu ya usalama barabarani kwa Umma,
2.    Utii wa sheria bila shuruti,
3.   Barabara salama (Safer Roads),
4.    Magari salama (Safer Vehicles),
5.   Usimamizi wa Sheria za Usalama barabarani (Traffic Management),
6.    Teknohama katika Usimamizi wa Usalama Barabarani,
7.    Uokoaji katika majanga ya ajali (Post Crash Response),
8.    Mradi wa Samarter Traffic,

Mkakati huo umeshapitiwa na vikao vikubwa vya maofisa wa Polisi Makao Makuu na kuupitisha uanze kutumika. Tuna imani iwapo mambo hayo yatatekezwa kama kamati ilivyopendekeza tunaweza kwenda sambasamba na mpango wa UN Decade of Action for Road Safety wa kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani kwa 50%.

MIKAKATI MINGINE NI KAMA IFUATAVYO:

    Kikosi cha Usalama Barabarani kwa nafasi ya pekee, kitaendelea kuwaelimisha na kuhamasisha waendesha pikipiki hasa wa bodaboda kufuata sheria za usalama barabarani kwa kuwa na leseni, uvaaji wa helmet, upakiaji wa abiria na uedeshaji salama wanapokuwa barabarani.

    Kuendelea kusimamia kwa makini zoezi la utoaji leseni za udereva. Kwa taarifa tu – Mradi wa utoaji leseni mpya za udereva ulianza rasmi tarehe 15/09/2010. Hadi kufikia tarehe 15/09/2012 leseni ambazo zimeshatolewa ni 535,709. Mchanganuo wa madaraja ya leseni yaliyotolewa hadi tarehe hiyo ni kama ifuatavyo:

    Daraja C - 15,955
    Daraja C1 - 54,465
    Daraja C2 – 52,246
    Daraja C3 – 51,574
    Daraja A – 306,059
    Daraja A1 – 15,269
    Daraja A2 – 34,757
    Daraja A3 – 3,283
    Daraja D – 498,169
    Daraja E- 263,322
    Daraja F – 32,089
    Daraja G – 50,002


NB: Kadi moja ya leseni inaweza kuwa na madaraja zaidi ya moja kutegemea na uwezo wa dereva kuendesha vyombo vya moto.

    Kuhakikisha kuwa mfumo wa kuweka nukta (point system) unaanza kutumika ili kuwadhibiti madereva wanaokithiri kwa makosa.

    Kuhakikisha mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (Car Tracking System) unaanzishwa ili kudhibiti mwendokasi.

    Tutaenelea kutumia vifaa vya kisasa kama Speed Radar/Laser, vipima ulevi katika usimamizi wa sheria.

    Tutaendelea kukagua vyuo vya udereva ili kuhakikisha vinatoa elimu bora itakayotupatia madereva wenye weledi.

    Kikosi kinaendelea kusimamia sheria za Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kufanya doria katika barabara kuu (Highway patrol) na barabara  za ndani ya mikoa ili kudhibiti makosa ya usalama barabarani. (tayari RTOs nchi nzima wameishatumiwa programu ya mwaka mzima ya uendeshaji operesheni).

    Kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wote wa barabara kwa njia ya Radio, Televisheni, shule za Msingi na Sekondari (tayari RTOs nchi nzima wametumiwa programu ya mwaka mzima  ya utoaji elimu), kupitia vipeperushi na majarida mbalimbali, kwenye maadhimisho mbalimbali kama ya sabasaba na kwenye vituo vya mabasi.

    Kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali wa usalama barabarani kwa lengo la kuboresha utendaji wa kazi za usalama barabarani ili kuleta dhana ya barabara salama na usalama barabarani.

MWISHO.