Wednesday, August 08, 2012

Wabunge Simba, Yanga 'wapigana vijembe'

Oliver Albert na Reginald Miruko, Dodoma
BAADHI ya wabunge wa Bunge la Muungano, jana waliligeuza Bunge, kama 'kijiwe' cha muda cha kupigana vijembe vya soka, wakati mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga walipotinga ndani ya Ukumbi wa Bunge  ili kutambulisha taji lao kwa mwaka wa pili mfululizo.
Yanga walitwaa taji la Kagame wiki mbili zilizopita, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali kwenye Uwanja wa Taifa, hiyo ikiwa ni mara ya pili, baada ya mwaka jana kufanya hivyo walipoifunga Simba bao 1-0 kwenye uwanja huo.
Vijembe hivyo vilianza muda mfupi baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kulitambulisha Bunge uwapo wa wachezaji na viongozi wa Yanga ndani ya ukumbi.
Wakati wabunge mashabiki wa Yanga wakilipuka kwa nderemo na vifijo kufuatia utambulisho huo, hali ilikuwa tofauti kwa wabunge mashabiki wa Simba ukumbini hapo.
Katika kujipoza, wabunge wa Simba, waliwajibu wenzao kwa kuwanyoshea mkono mmoja, ikiwa ni ishara kuwakumbusha kipigo cha mabao 5-0 walichopata kwenye mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita.
Pamoja na uchache wao bungeni na kufunikwa na makofi na kelele za wabunge mashabiki wa Yanga, bado wabunge mashabiki wa Simba hawakuwa nyuma kuwajibu.
Kelele za 'tano bila...tano bila', zilisikika kutoka kwa baadhi ya wabunge wapenzi wa Simba, huku wale wa Yanga wakionyesha ishara ya mkono mmoja (maama yake ni kwamba Yanga imetwaa Kombe la Kagame mara tano).
Aliyekuwa wa kwanza kunyoosha mkono, ni Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage (Mbunge Tabora Mjini) kisha kufuatiwa na mbunge kijana Joshua Nassari (Arumeru) ambaye mbali na kunyosha mkono, alisema: "Tano bila... tano bila."
Awali, wakati akiwatambulisha Yanga, Spika Makinda aliwapongeza kwa kufanikiwa kutwaa taji hilo kubwa la vilabu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
"Jamani kama  watu wameleta kitu kizuri bungeni lazima niwapongeze...Yanga hongereni sana," alisema Makinda na kushangiliwa na wabunge mashabiki wa Yanga.
Aliongeza: "Lakini acheni tabia kwamba, kwa sababu nimetoa pongezi, basi mimi ni shabiki wa Yanga...siku nyingine nikiwapongeza Simba, mtasema mimi ni Simba."
Nje ya Ukumbi wa Bunge, jana hiyo kulifanyika sherehe ya kuzindua tawi jipya la wabunge wanachama wa Yanga, ambapo wachezaji na viongozi wa klabu hiyo ya Jangwani walishiriki.
Sherehe hizo zilifanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, ambapo mgeni rasmi alikuwa Fatma Karume. Mbunge Mohamed Misanga (Singida Magharibi), alichaguliwa kuwa mwenyekiti, huku nafasi ya Katibu ikienda kwa Geofrey Zambi (Mbozi).


Source:Mwananchi