Imesema pamoja na mambo mengine, imefikia hatua hiyo ili kuondoa malalamiko yaliyokuwa yamejitokeza kwa wafanyakazi na wanachama wa mifuko hiyo, baada ya sheria hiyo kuanza kutekelezwa.
Taarifa hiyo, ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.
"Kabla ya kuhitimisha hoja yangu, naomba kutoa maelezo mafupi kuhusu Azimio la Bunge lililowasilishwa hapa jana na mheshimiwa Seleman Jafo, Mbunge wa Kisarawe juu ya umuhimu wa kuletwa bungeni Muswada wa dharura wa Marekebisho ya Sheria namba 5 ya mwaka 2012, inayozungumzia marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambayo ndani yake, imeeleza kuzuiwa kwa fao la kujitoa kwa wafanyakazi.
"Sheria hii, ilipoanza kutumika ilitafsiriwa kwa njia tofauti na hata vyombo vya habari viliripoti kwa njia tofauti. Wapo waliosema mifuko yetu, inataka kufilisika na wengine wanasema mfumo huu umeanzishwa na CCM ili ipate fedha kwa ajili ya matumizi ya kisiasa.
"Hayo yote siyo kweli, tatizo lililoko hapa wakati mabadiliko haya yanakuja, hatukutoa elimu kwa wadau ndiyo maana malalamiko yamekuwapo.
"Katika hili, namshukuru mheshimiwa Jafo, kwa sababu amezunguka katika migodi mbalimbali, ikiwamo Geita, Bulyanhulu na Nyamongo ambako alizungumza na wafanyakazi.
"Kutokana na malalamiko kuwa mengi, Serikali imekubali kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo hapa bungeni, ili ujadiliwe kwa undani na nasema mchakato wa muswada huu, utapita hatua zote na tutatoa elimu kwa wadau ili waelewe," alisema Waziri Kabaka.
Kwa mujibu wa waziri huyo, utaratibu wa wafanyakazi kujitoa na kuchukua mafao yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii, umekuwapo kwa muda mrefu na ulihusu wafanyakazi wote wa mikataba ya ajira ya masharti ya kudumu na malipo ya pensheni pamoja na wale wa mikataba ya masharti ya muda maalum.
Awali Msemaji wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama (CCM) alisema baada ya sheria hiyo kurekebishwa mafao ya kujitoa yarejeshwe na pia wanachama waruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yao ya uzeeni kulipia mkopo wa nyumba.
Alitaka wanachama waruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yao ya uzeeni kugharamia shughuli yoyote nyingine, kwa lengo la kuandaa mazingira mazuri ya maisha baada ya kustaafu.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Kawawa (CCM), aliitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA), ifanye kazi kwa uangalifu, ili kuondoa malalamiko kwa wafanyakazi.
Mtanzania