Wakubwa wanavyotafuna nchi
*Kampuni ya Mohamed Enterprises yauziwa viwanja kinyemela
*Bandari watumbua zaidi ya bilioni 1.5, waendesha miradi hewa
*Mabosi wanachomeka watumishi hewa, wanavuta mishahara
Na Manyerere Jackton, Dodoma
Ripoti
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick
Utouh, ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2011; imeendelea kufichua
namna kundi la watumishi wa umma na wafanyabiashara wakubwa
wanavyoitafuna Tanzania. Utouh aliwasilisha taarifa hiyo bungeni
mwishoni mwa wiki.
Fedha
na mali za umma zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ama zinaibwa au
zinachukuliwa kwa namna ambayo ni vigumu kuamini kama kweli viongozi
wakuu wa kitaifa wana dhamira ya kutokomeza ufisadi uliovuka mipaka.
Kuuzwa kwa viwanja, majengo ya Serikali
CAG
amebaini kuwa kiwanja kilichopo katika Kitalu Na. 10 katika Barabara ya
Nyerere, kimeuzwa kwa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited
(MeTL) kinyemela. Amesema wakati uuzaji kiwanja hicho ulipaswa uratibiwe
na Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC - mrithi wa PSRC),
kazi hiyo ilifanywa na watu wasiokuwa na mamlaka kisheria.
Nyaraka
za mawasiliano kati ya MeTL, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina
zinazohusiana na uuzaji kiwanja hicho, zinaonyesha kuwa Wizara ya Fedha
na Msajili wa Hazina ndiyo waliojihusisha moja kwa moja katika uuzaji wa
mali hiyo ya umma, kwa kutoa maelekezo kwenye menejimenti ya CHC. Bodi
ya Wakurugenzi haikushirikishwa kabisa.
Hatimaye
kiwanja hicho kiliuzwa kwa MeTL kwa Sh bilioni 2.046 bila kufuatwa kwa
Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005.
Katibu wa Waziri aamuru kampuni ilipwe Sh bilioni 2.34
Utata
wa matumizi mabaya ya fedha za umma, umemkumba aliyekuwa Katibu wa
Waziri mwenye dhamana ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kuhusu kiwanja
namba 192 kilichopo Barabara ya Nyerere. Alimwandikia barua Mwenyekiti
wa PSRC ailipe kampuni ya DRTC Sh milioni 954.72.
Hata
hivyo, Meneja Mkuu wa DRTC akamwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC
akitaka alipwe haraka kiasi cha Sh bilioni 2.349. Kwenye barua hiyo,
Meneja wa DRTC alisisitiza kuwa malipo hayo ni maelekezo kutoka
serikalini, licha ya ukweli kwamba yalikuwa ni makubwa kuliko madai
halisi na akalipwa.
Kuuzwa kwa jengo la kampuni ya umma ya TMSC
Jengo
la kampuni ya Tanzania Motors Services (TMSC) lipo katika kitalu namba
24 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam.
Jengo
hilo liliuzwa kwa kwa kampuni ya Saddiq Super Service Station (SSSS)
kwa Sh bilioni 1.3. Kampuni hiyo ilitoa malipo ya awali ya asilimia 10,
yaani Sh milioni 130. Baadaye Wizara ya Fedha ikaitaarifu CHC kuwa
Serikali imeghairi kuliuza jengo hilo lililopo kitalu namba 24 kwa
kampuni ya SSSS. Wizara ya Fedha ikaitaka CHC ikubaliane na SSSS
kuwafidia, kwani tayari kampuni hiyo ilishatoa kianzio cha Sh milioni
130.
Kuona
hivyo, kampuni ya SSSS ikawasilisha madai ya kulipwa fidia ya Sh
bilioni 3.894 kwa ajili ya kupoteza biashara yake na Sh milioni 500 kama
fidia kwa usumbufu. Hatimaye ikaamuliwa kuwa SSSS ilipwe Sh milioni 964
ambamo ndani yake kulikuwa na Sh milioni 130 ilizotoa awali na gharama
za usumbufu.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha alikuwa Mwenyekiti wa kikao kilichoidhinisha
malipo hayo. Akawasilisha katika Wizara ya Fedha ambayo yeye ni
kiongozi, ili ilipe kiasi hicho cha fedha kwa maelekezo ya kikao
alichokiongoza yeye mwenyewe.
Kwa
uamuzi huo, Wizara ya Fedha ikailipa moja kwa moja SSSS Sh milioni
964.2; ilhali kama ni malipo, basi yalipaswa kufanywa na CHC. Malipo
hayo, kwa mujibu wa taarifa ya CAG, yanaibua maswali juu ya dhamira ya
Wizara ya Fedha kulipa fedha hizo haraka haraka bila kuishirikisha
Menejimenti wala Bodi ya Wakurugenzi ya CHC.
Malipo ya kushangaza kwa kampuni ya Tantrack
Tantrack
Agencies ilikuwa mpangaji katika jengo la TMSC lilipo kitalu namba 24,
Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Ilipanga kwa miaka miwili
kuanzia Julai Mosi 1993. Kampuni hiyo inasema ilitumia Sh milioni 24
kukarabati jengo kwa wakati wote wa mkataba wake wa upangaji, licha ya
ukweli kwamba jambo hilo halikuwamo kwenye mkataba iliyoingia na TMSC.
Ikakataa kulipa ada ya pango ikisema fedha hizo zilizotumika kwenye
ukarabati zitambuliwe kuwa ndiyo ada ya pango.
Tantrack
ikafungua kesi ya madai namba 257 ya mwaka 1995 katika Baraza la Nyumba
Mkoa wa Dar es Salaam (DRHT) dhidi ya TMSC, kwa kigezo kwamba TMSC
ilikuwa ikivunja makubaliano. Ilifanya hivyo baada ya TMSC kuiandikia
barua ikiipa notisi ya miezi sita ihame kutokana na kutotekeleza
makubaliano ya mkataba.
Wakati
hayo yakiendelea, jengo la TMSC likauzwa kwa njia ya mnada kwa African
Terminal Limited (ATL) kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam, kwa Sh milioni 3. CHC ikapeleka vielelezo vyake mahakamani
ikionyesha mkataba ulivyokuwa kati yake na Tantrack. Kabla rufaa
haijasikilizwa, ATL ikaweka pingamizi. Sasa ni miaka 15 suala hilo
likiwa halijaamuliwa.
CAG anasema imebainika kuwa kuna uzembe na kutowajibika kwa pande zote mbili zinazopambana kwenye mgogoro huo.
Utata Kitalu namba 33 kilichotwaliwa na Kampuni ya Maungu Seeds
PSRC
iliingia makubaliano na kampuni ya Maungu Seeds, kwa ajili ya kununua
kiwanda cha Mzizima Maize Mill kilichopo Kitalu namba 33, Barabara ya
Saza katika Eneo la Viwanda Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Makubaliano
hayo yalitiwa saini Septemba 1, 2004; na gharama ya ununuzi ilikuwa Sh
milioni 620. Malipo yalikuwa yafanywe kwa awamu tatu. Maungu ikaanza
kulipa Sh milioni 200 na kutoa dhamana ya benki (TIB) ya Sh milioni 420.
Ikakubaliwa
kuwa PSRC ingeikabidhi kampuni ya Maungu kiwanda hicho ndani ya miezi
mitatu baada ya kutiliana saini ya ununuzi, na kwamba Maungu
ingekabidhiwa nyaraka zote baada ya kukamilisha malipo. Iliyokuwa PSRC
ikashindwa kukabidhi kiwanda kwa mujibu wa makubaliano kwenye mkataba
kutokana na kwamba, kiwanda kilikuwa rehani kwa kampuni ya CDC London ya
Uingereza tangu mwaka 1959.
Hatimaye,
ilipofika Aprili 26, 2006 rehani ikawa imeondolewa, lakini tayari muda
wa dhamana ya benki ulikuwa umekwisha. Kiasi cha Sh milioni 420 kikawa
hakijalipwa. Mwaka 2010 kampuni ya Maungu ikafungua kesi ya madai na
ikaamuriwa kuwa ipewe hati ya eneo yenye namba 6639. PSRC (CHC)
ikaamuriwa iilipe Maungu Sh milioni 200 haraka. Fedha hizo ni zilezile
ilizokuwa imetoa kama malipo ya awali na ikarejeshewa.
Kimsingi,
Maungu ikawa haijalipa chochote, lakini ikawa imepewa kiwanda cha
Mzizima bure kabisa bila kulipa kiasi chochote kwa mali hiyo ya umma.
Madeni ya Simu 2000 yafutwa kienyeji
CAG
ameonyesha wasiwasi mkubwa kwa uamuzi wa CHC wa kufuta madeni mengi ya
iliyokuwa kampuni ya Simu 2000. Kampuni hiyo iliundwa na kuongozwa na
familia ya Mama Anna Mkapa, kwa ajili ya kuuza zilizokuwa mali za
Shirika la Posta na Simu. Kuna habari kwamba familia hiyo ilijitwalia
mali kadhaa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Miongoni mwa majengo
yaliyouzwa ni maghorofa yaliyopo Ilala.
Ulaji Chuo cha Ubaharia (DMI)
Ukaguzi
uliofanywa na CAG umebaini kuwa Sh milioni 83.96 zimelipwa kama takrima
na fedha za kujikimu kwa viongozi bila kuidhinishwa na mamlaka za
kisheria. Katika malipo hayo, maofisa wa Wizara ya Mawasiliano walilipwa
Sh milioni 12; na Sh milioni 51.8 zililipwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la
DMI kama posho ya madaraka (honorarium), mafuta na posho ya vikao.
Sh
milioni 2.6 zililipwa kwa maofisa wa akaunti wa DMI bila wao wenyewe
kuhudhuria vikao; Sh. milioni 10.4 zililipwa kwa watumishi wa DMI kama
posho ya kujikimu Juni, 2009 bila wenyewe kuhudhuria kile kilichoitwa
kuwa ni kikao cha kikosi kazi cha kupitia mitaala ya DMI.
Katika
hatua nyingine, DMI ilipokea Sh milioni 385 kwa ajili ya kuwalipa
wadeni wake, lakini ukaguzi umebaini kuwa ni 205.8 pekee zilizotumika.
Wafanyakazi 12 wa DMI wamelipwa mishahara ya ngazi ya PGSS 5 na zaidi
bila kuidhinishwa na Baraza DMI. Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala
amekuwa akijilipa mshahara kwa kiwango cha PHTS ambacho
hakikuidhinishwa.
Kompyuta za msaada zaibwa, zanyofolewa vifaa
Ukaguzi
umebaini kuwa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, kilitoa msaada wa
kompyuta 25 kwa DMI kwa ajili ya maktaba yake. DMI ilimlipa wakala wa
utoaji vifaa hivyo bandarini Sh milioni tatu Desemba 7, 2007. Lakini
hadi ukaguzi unafanywa, kompyuta hizo zilikuwa hazijawasilishwa kama
ilivyotarajiwa.
Baadaye
imebainika kuwa kati ya kompyuta hizo, ni kompyuta 13 pekee
zilizowasilishwa katika maktaba, na kwamba ni kompyuta nne pekee
zinazoweza kukarabatiwa. Kompyuta kenda haziwezi kutengenezwa kutokana
na kuibwa vifaa muhimu kama Ram, Processors, Hard disks, Power Supply na
Mother Boards.
Bohari ya Dawa (MSD) inaingiza vifaa feki
Pamoja
na kuwapo upotevu wa mamilioni ya shilingi zinazotolewa kwa ajili ya
ununuzi wa dawa, CAG amebaini kuwa baadhi ya vifaa na dawa
vinavyosambazwa na MSD havina ubora. Ametoa mfano wa mashine za kupima
shinikizo la damu na vifaa vinavyotumika kubebea wagonjwa.
Pia
dawa kama kwinini imebainika kuwa inasambazwa nyingine ikiwa na ubora
wa hali ya chini, kutokana na pengine kutohifadhiwa vizuri. Aidha,
ukaguzi umebaini kuwa vitambaa vinavyotumika kunyonya damu wakati wa
upasuaji huwa vipo chini ya kiwango.
Ukaguzi
umebaini kuwa Sh bilioni 3.95, dola milioni 9.4 na euro milioni 1.5
ambazo zimetumika bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya MSD na hivyo
kukiuka Sheri ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni 41 ya Tangazo
la Serikali namba 97.
Aidha,
imebainika kuwa MSD imefanya ununuzi kwa zabuni nane huku upitiaji wa
zabuni hiyo ukifanywa na mtu mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Zabuni zilizofikwa na hali hiyo ni za Sh milioni 134.4, dola 10,000 na
Euro milioni 1.5.
Ulaji wa kutisha Bandari ya Dar es Salaam
Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba na kampuni ya Singapore PTE
Limited kwa ajili ya kuweka ‘Radio Data Terminals’ Februari 2010 wenye
thamani ya dola 339,600. Punde tu baada ya TPA kupata radio hizo, mambo
kadhaa yalianza kujitokeza.
Kwanza, menejimenti ikabaini kuwa ‘Radio Data Terminals’ hizo haziwezi
kufanya kazi bila kile kinachoitwa kitaalamu kuwa ni ‘Access Points’
(virusha mawimbi). Hatua hiyo ikaifanya PTA iingie mkataba mwingine na
Singapore PTE Limited Juni 21, 2010 kwa ajili ya kuweka virusha mawimbi
68 kwa gharama ya dola 399,000.
Baada
ya kununua vifaa hivyo, ikabainika tena kwamba haviwezi kufungwa juu
minara ya iliyokuwapo. Kwa sababu hiyo, PTA ikaingia mkataba mwingine na
CATS (T) Limited Septemba 17, 2010 kwa ajili ya kuweka minara mingine
kwa gharama ya dola 133,000.
CAG
anasema katika ukaguzi wake kwamba pamoja na kufanya yote hayo, bado
‘Radio Data Terminals’ hazikuweza kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, kwa
vile ilipaswa iunganishwe kwenye mkongo (fibre optic) kwa gharama ya
dola 553,800 za Marekani. Kazi hiyo ikafanywa na EMEC.
Kwa
kifupi, TPA ikajiingiza kwenye gharama za ziada za dola milioni 1.09 na
bado kilichokusudiwa hakikuweza kupatikana kwa muda kutoka kwa
mkandarasi aitwaye CATS. Hakuna gharama zozote ambazo TPA imeweza
kuzidai kutokana na kucheleweshwa au kuingia gharama kubwa kiasi hicho.
Hii inatiliwa shaka kuwa ndiyo ulaji wenyewe.
Sh milioni 100 zaliwa bila jengo la bosi TPA
TPA
iliingia mkataba na kampuni ya AF MULT-CON LIMITED kujenga makazi ya
Meneja wa Bandari Tanga kwa gharama ya Sh milioni 500. Utangazaji zabuni
umebainika kuwa ulifuata taratibu zote. Hata hivyo, CAG amebaini kuwa
kuna uzembe katika kufuatilia taratibu za mkataba wa zabuni. CAG
mwenyewe alizuru eneo lililokusudiwa kujengwa jengo hilo, na
hakushuhudia malighafi wala shughuli yoyote ya kuhalalisha malipo ya Sh
milioni 100 ambazo tayari mzabuni alishalipwa.
Mkataba mwingine wa utata TPA
Wakati
wa ukaguzi, CAG alibaini kuwa TPA iliingia mkataba na kampuni ya
Chibeshi Construction kwa ajili ya kujenga uzio katika kitalu namba moja
kwenye Bandari ya Mtwara. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh milioni
679.8. Ulitiwa saini Aprili 14, 2009 na ujenzi ulipaswa ukamilike kwa
wiki 26 kutoka siku ya kutiwa saini mkataba.
Kabla
ya mkandarasi kuanza ujenzi, TPA ikaamua kuvunja mkataba huo kwa
maelezo kwamba hapakuwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Uamuzi huo ukaifanya TPA iingie hasara ya Sh milioni 92.6 kama adhabu au
faini. Ikamlipa mkandarasi. Fedha zikachukuliwa na mkandarasi bila
kufanya kazi yoyote.
Mkataba mwingine wa utata waingiza hasara TPA
Katika
ukaguzi, CAG amebaini kuwa PTA iliingia mkataba na kampuni ya WiA kwa
ajili ya kuweka mawasiliano ya intaneti katika Makao Makuu ya TPA, na
bandari nyingine zilizo chini ya Mamlaka hiyo. Mkataba huo ulikuwa wa
miezi mitatu kuanzia Julai 2010.
Hata
hivyo, mradi huo haukukamilika baada ya muda uliopangwa kumalizika. TPA
ikaamua kumwongeza mkandarasi muda hadi Februari 28, 2011 na mkandarasi
bado alishindwa. TPA ilipaswa kumtoza mkandarasi kiasi cha dola 95,000
kwa kushindwa kutekeleza mkataba kwa muda, lakini haikufanya hivyo.
Hazina yalipa mamilioni ya mishahara hewa
Wakati
wa ukaguzi, CAG amebaini kuwa Hazina imeendelea kutumia mamilioni ya
shilingi kuwalipa wafanyakazi hewa katika taasisi mbalimbali. Katika
ukaguzi huo, imebainika kuwa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) kumekuwa na
majina 42 ya watu wanaolipwa mishahara licha ya ukweli kwamba si
watumishi wa chuo hicho. Imebainika kuwa kuanzia Oktoba 2009 hadi Juni,
2010 MUCE ilipokea Sh milioni 612 na kuwalipa watumishi hewa.
Katika
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Hazina imeendelea
kuwalipa mishahara watu ambao si watumishi chuoni hapo. Baadhi ya
waliostaafu na MNMA kupeleka majina yao Hazina, wanaendelea kulipwa.
Hali hiyo imesababisha Sh milioni 134.74 zitumike kuwalipa watu ambao si
watumishi katika chuo hicho. Fedha hizo hazikurejeshwa Hazina.
Katika
Chuo Kikuu cha Mzumbe, orodha ya majina kutoka Hazina inaonyesha kuwa
hata wale ambao si watumishi tena wa chuo hicho, majina yao yapo kwenye
orodha ya wanaostahili kulipwa mishahara. Kuanzi Oktoba 2010, Machi
2011, Mei 2011 na Juni 2011 Sh milioni 194.4 zimetumika kuwalipa watu
ambao si watumishi katika chuo hicho.
Imebainika
pia kwamba baadhi ya watumishi waliojiuzulu au kuacha kazi katika Chuo
cha Ustawi wa Jamii (ISW), majina yao yameendelea kuwa kwenye orodha ya
Hazina ya watumishi wanaopaswa kulipwa. Sh milioni 181 zilikuwa
zimetumika kuwalipa hadi wakati ambao CAG alikuwa akiandaa ripoti hii.
Katika
Chuo cha Elimu Dar es Salaam nako mambo ni kama hayo. Watu 56 ambao
hawapo kwenye utumishi wameweza kulipwa Sh milioni 778.7 licha ya ukweli
kwamba hawapo chuoni hapo. Hakuna rekodi inayoonyesha kuwa fedha hizo
zilirejeshwa Hazina.
Fedha za Mifuko ya Jamii hatarini
Ukaguzi
umebaini kuwa upo udhaifu mkubwa na hatari ya kupotea kwa mabilioni ya
shilingi zilizowekezwa na Mifuko ya Jamii katika miradi mbalimbali
nchini.
Shirika
la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetumia Sh bilioni 234.054 kwa ajili ya
ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Kati ya fedha hizo, ni Sh bilioni
35.218 pekee ambazo zilisainiwa katika ujenzi wakati wa awamu ya kwanza.
Fedha zilizotolewa katika ujenzi wa awamu ya pili, hazikusainiwa.
Majengo ya awamu ya kwanza yamekamilika, lakini Serikali haijaanza
kurejesha fedha inazodaiwa na NSSF zenye riba ya Sh bilioni 14.157.
Wabunge waondolewe kwenye Bodi
Kwa
mara nyingine, CAG amependekeza wabunge wasiwemo kwenye Bodi za
Mashirika ya Umma na bodi nyingine. Anasema mapendekezo hayo yanatokana
na ukweli kwamba kuwamo kwao kwenye bodi husababisha mgongano wa
masilahi.
Anasema
ni Tanzania pekee ambayo wabunge ni wajumbe katika bodi za mashirika ya
aina hiyo. Utaratibu kama huo haupatikani mahali kwingineko duniani
wala katika vyombo ambavyo Tanzania ni mwanachama.
Uteuzi wa wajumbe wa Bodi
CAG
anatoa mapendekezo kwamba maofisa watendaji wakuu wa kampuni/mashirika
ni vizuri wakateuliwa na Bodi za Wakurugenzi badala ya utaratibu wa
sasa, ambako ni Rais anayewateua. Anapendekeza Rais aachiwe madaraka ya
kuteua mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi.
Mapendekezo
hayo, kwa mujibu wa CAG, yanalenga kuifanya Bodi ya Wakurugenzi iweze
kuisimamia vema menejimenti na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa.
Serikali ibane ununuzi mashangingi
CAG
anapendekeza kuwa ili fedha nyingi zielekezwe kwenye maendeleo,
Serikali haina budi kuweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi
hasa kwenye ununuzi wa magari ya kifahari, gharama za semina na
kupunguza idadi ya wanaosafiri kwenye misafara ya viongozi ndani na nje
ya nchi.
…tamati
@@@……
Source: Gazeti la Jamhuri