Na kitengo cha Sheria na Mahusiano,
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
TIMU ya Uchukuzi Sports Club imepania kufanya vyema kwenye mashindano ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yatakayofanyika mjini Dodoma kuanzia Aprili 16 mwaka huu.
Mwenyekiti wa timu hiyo inayoundwa na wafanyakazi wa taasisi zinazounda Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mohamed Ally alisema kuwa timu yake itafanya vizuri katika mashindano hayo, kutokana na maandalizi kabambe waliyofanya.
Ally alisema kuwa kwa sasa wako katika mazoezi makali kujiandaa na mashindano hayo, ambayo yatafikia kilele siku ya Mei Mosi mjini Dodoma.
Ally alisema Uchukuzi Sports Club inaundwa na timu za michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, bao, karata, riadha, baiskeli na vishale.
Alisema kuwa wana uhakika timu yao kufanya vizuri katika mashindano hayo, kutokana na kufanya mazoezi kwa muda mrefu chini ya makocha wazoefu wa michezo hiyo.
Ally aliwataja baadhi ya makocha hao kwa upande wa soka kuwa ni pamoja na Kenny Mwaisabula, Robert Damian, Terry, Kingsley Malwilo na Abunu Issa, ambao wameifanya timu yao kuwa tishio kwa timu zingine, wakati netiboli inafundishwa na mchezaji mkongwe Judith Ilunda.
Alisema kuwa timu zao hizo zimekuwa zikicheza mechi za kirafiki na timu mbalimbali, ili kuwawezesha makocha kubaini makosa na kufanya marekebisho ya mwisho kabla timu hiyo haijaondoka kwenda Dodoma.
Naye Meneja wa Uchukuzi Sports Club, Robert Damiani alisema kuwa timu yao inatarajia kwenda Dodoma Aprili 14 tayari kwa mashindano hayo.
Damiani alisema wanauhakika wa kufanya vizuri na kuvunja rekodi ya mwaka jana ya kutwaa vikombe 13, kati ya hivyo vitano vikiwa ni vya ushindi wa kwanza, wakati vilivyosalia walishika nafasi ya pili na tatu.
Timu ya soka ya Uchukuzi Sports Club iliyopo chini ya Wizara ya Ujezi, Uchukuzi na Mawasiliano ikifanya mazoezi wakijiandaa kwa mashindano ya Mei Mosi
Makipa wakila tizi maalumu
Kikosi kabambe cha timu ya soka ya Uchukuzi kikiwa pamoja na kocha na meneja wa timu hiyo Robert Damiani (kushoto).
Wachezaji wa timu ya wanawake ya kuvuta kamba ikiwa kwenye mazoezi katika viwanja vya JNIA.
Kikosi kabambe cha wanawake cha klabu ya Uchukuzi wakifanya mazoezi kabla ya kuvuta kamba.