Monday, April 25, 2016

MATUKIO YA UBAKAJI YAONGEZEKA NA KUFIKIA 1765.



MATUKIO YA UBAKAJI YAONGEZEKA NA KUFIKIA 1765.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
                         WIZARA YA MAMBO YA NDANI
                   JESHI LA POLISI TANZANIA
 
 Matukio ya ubakaji hasa kwa watoto wadogo yamekuwa yakiongezeka kwa kiwango kikubwa, ongezeko hili limebainika kutokana na ufuatiliaji tulioufanya kupitia matukio yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi ambapo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016 kumeripotiwa matukio 1765 ukilinganisha na matukio 1585 katika kipindi kama hicho mwaka 2015 ikiwa ni ongezeko la matukio 180.

Katika matukio ya Januari hadi machi 2016, jumla ya watuhumiwa 823 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ingawa bado kumekuwa na tabia ya wazazi na walezi kuficha watuhumiwa wa ubakaji na  kumaliza kesi hizo kirafiki au kifamilia jambo ambalo ni kinyume cha sheria bila kuzingatia madhara aliyoyapata mtoto.

Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linakemea vikali wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu vya ubakaji na wazazi ama walezi wanaofumbia macho vitendo hivyo na kuingia makubalino na watuhumiwa kwa kupeana fedha kama fidia ili wamalize kesi kiundugu au kifamilia.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa  Wazazi, walezi, Viongozi wa dini, Asasi za kiraia, walimu na Wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano katika kushughulikia vitendo hivyo ikiwemo kuwafichua wazazi au walezi wanaofanya makubaliano ya kumaliza kesi za ubakaji kirafiki au kifamilia ili kukomesha vitendo hivyo.

 Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

Makao Makuu ya Polisi.