ILI kukabiliana na ukame, kupiga vita jangwa na utunzaji wa mazingira, shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ina mpango wa kupanda zaidi ya miti 1,500 kwenye eneo hilo.
Akizungumza na wageni waliotembelea shule hiyo Megan Allen kutoka Marekani na Juliane Friedrich wa Ujerumani, meneja wa shule hiyo Monica Mlemeta, alisema wao ni wana mazingira, hivyo wataendelea kupanda miti mingi zaidi japo eneo hilo waliloligeuza kuwa la kijani tofauti na awali.
Mlemeta alisema shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, ina lengo la kuanzisha kidato cha tano hadi cha sita, ili kuboresha elimu ya eneo hilo la Simanjiro pamoja na kuzidi kutunza mazingira kwa kupanda miti mingi.
Alisema japokuwa wanatumia gharama kubwa kupanda miti katika eneo hilo kutokana na jiografia iliyopo ikiwemo kutoa udongo sehemu nyingine, watahakikisha wanabadili mandhari ya eneo kwa kuotesha miti zaidi.
Mratibu wa asasi ya Community Education resources foundation, Godfrey Lema walioipatia shule ya Mgutwa miti hiyo 1,500 alisema lengo lao ni kuhakikisha wanatunza mazingira na kuondokana na ukame uliopo katika eneo hilo.
Alisema kwa kushirikiana na asasi za Nick's Eco safaris na Moivaro Jitegemee Family wamefanikisha hilo, japo ardhi ya eneo hilo ina mwamba na magadi, uongozi wa shule umelibadili kuwa la kijani, kwa kuendeleza utunzaji mazingira na kuwa mfano wa kuigwa.
"Wageni wetu Megan Allen kutoka Marekani na Juliane Friedrich wa Ujerumani, wamefurahia ukijani uliopo hapa na tutahakikisha tunaendelea kuiunga mkono shule hii, kwani imekuwa mfano bora wa utunzaji mazingira," alisema Lema.
Alisema elimu ya mazingira inatakiwa kutolewa kwa sehemu kubwa ya jamii ya wananchi wa wilaya ya simanjiro, ili kuhakisha wanapanda miti kwa wingi kwani ndiyo vyanzo vya mvua na kupata kivuli, matunda na hewa safi.
Wageni mbalimbali wakiwemo Megan Allen wa Marekani na Juliane Friedrich wa Ujerumani, walioitembelea shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiangalia baadhi ya miche ambayo itapandwa kwenye shule hiyo. Mwalimu wa mazingira wa shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Kata ya Shambarai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Godlove Issa (kushoto) akiwaonyesha wageni walioitembelea shule hiyo, baadhi ya miche inayotarajiwa kupandwa ili kutunza mazingira.
Mwalimu wa mazingira wa shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Kata ya Shambarai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Godlove Issa na raia wa Marekani Megan Allen, wakipanda mti kwenye shule hiyo ili kutunza mazingira.