Monday, December 15, 2014

TANZANIA ONE YANUNULIWA NA WATANZANIA



TANZANIA ONE YANUNULIWA NA WATANZANIA
KAMPUNI ya Richland Resource yenye makao yake nchini Uingereza ambayo pia inamiliki kampuni tanzu la Tanzanite One iliyopo Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara imeuza hisa zake zote kwa Kampuni ya Sky Associates Group inayomilikiwa na Watanzania.



Richland ambayo inaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bernard Oliver imeamua kuuza hisa zake asilimia 50 kwa wazawa hao kutokana na Kampuni ya Tanzanite One kukumbwa na madeni na kushindwa kujiendesha na kukabiliwa na deni la Sh bilioni 23.
Taarifa za kibiashara zilizotumwa na Kampuni ya Richland katika mtandao wake nchini Uingereza na kuthibitishwa na wakurugenzi wote wa kampuni ya Sky Associates Group, Hussein Gonga na Faisal Shahbhati zilisema kuwa kushindwa kujiendesha kwa kampuni ya Tanzanite One ni kutokana na migogoro kati ya kampuni hiyo na wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakivamia migodi hiyo mara kwa mara na hakuna ulinzi madhubuti.
"Tumeamua kuuza hisa zetu kwa Sky Associates Group kampuni inayoongozwa na Watanzania kwa asilimia 100, baada ya kuona uzalishaji ni mdogo na ulinzi dhidi ya mali na wafanyakazi unatia shaka," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mbali ya Gonga na Shahbhati, Mkurugenzi mwingine aliyemo katika Kampuni ya Sky Associates iliyonunua hisa za Tanzanite One, Rizwan Ullah raia wa India anamiliki hisa kidogo tu katika kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuona baadhi ya nyaraka zilisema kuwa Sky Associates Group imenunua hisa za Tanzanite One na mali za kampuni hiyo kwa thamani ya zaidi ya Sh bilioni 32 fedha za Kitanzania.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tayari Kampuni ya Sky Associates Group imechalipa Sh bilioni 27 ikiwa ni pamoja na madeni na kumiliki mali za kampuni ya Tanzanite One na bado inadaiwa dola za kimarekani milioni 5.1 sawa na fedha za kitanzania Sh bilioni 8.9 Habari za ndani ya Kampuni ya Tanzanite One zinasema kuwa madeni makubwa yanayoikabili kampuni hiyo ni pamoja na taasisi za serikali na wabia wengine wa kampuni hiyo na kufikia kiwango hicho cha Sh bilioni 23.
Uchunguzi umebaini pia kuwa Kampuni ya Sky Associates Group mbali ya kumilikiwa na wazawa kwa asilimia 100 lakini imesajiliwa nchini Hong Kong na wakurugenzi wa kampuni hiyo wamekuwa wakifanya biashara ya madini katika nchi mbalimbali duniani.
Akizungumzia kununua hisa za kampuni ya Tanzanite One, mmoja wa wakurugenzi wa Sky Associates, Hussein Gonga alikiri yeye na mwenzake Faisal kununua hisa za Tanzanite One na hisa nyingine asilimia 100 kumilikiwa na serikali.
Gonga alisema; "Kwa sasa ninachoweza kusema ni kweli kampuni yangu imenunua hisa zote za Tanzanite One na kuna taratibu nyingine za kisheria zinafuata na taratibu hizo zikikamilika tutatoa taarifa rasmi. "Tumelazimika kuigomboa Tanzanite One kwa kununua hisa zake baada ya kukabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni na kushindwa kujiendesha kibiashara," alisema Gonga.