Msimamizi msaidizi wa uchaguzi kitongoji cha Msikitini kwenye Kijiji cha Mbwewe wilaya ya Bagamoyo Said Mlinde kulia akiongea na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alipotembela kituo hicho kushuhudia zoezi la upigaji kura.
msimamizi msaidizi wa kituo cha kupigia kura Kitongoji cha Mkwajuni kwenye Kijiji cha Miono wilaya ya Bagamoyo Faustina Oforo akisubiria wapiga kura wa uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa uchaguzi uliofanyika juzi.
Na John Gagarini, Bagamoyo.
HUKU uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ukiwa umefanyika juzi na matokeo yakiendelea kutoka wananchi 514 wa Kijiji cha Mwetemo Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo wameshindwa kupiga kura kutokana na uhaba wa karatasi za kupigia kura.
Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika kutokana na karatasi za kupigia kura kuwa chache hivyo watu wengine kushindwa kupiga kura ambapo watafanya uchaguzi huo Desemba 19.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kitongoji hicho kuangalia zoezi hilo la upigaji kura wa kuchagua viongozi akiwemo mwenyekiti na wajumbe watano msimamizi msaidizi wa uchaguzi Thomas Madega alisema kuwa wamekubaliana uchaguzi huo kufanyika siku hiyo.
"Karatasi za kupigia kura kwanza zilichelewa kwani zilifika kituoni saa 10 kasoro jioni na pia zilikuwa chache hivyo watu wachache walipiga kura na wengine walishindwa kupiga kabisa," alisema Madega.
Madega alisema kuwa walikaa na viongozi wa vyama vyote na kukubaliana kusogezwa mbele zoezi la upigaji kura. "Tumekubaliana na vyama vyote kusogeza uchaguzi huo hadi Ijumaa na wamekubali tumewaambia wawatangazie wafuasi wao juu ya hili," alisema Madega.
Juu ya kuahirisha kwa muda mrefu tofauti na maeneo mengine ambayo yalikuwa na matatizo na uchaguzi kufanyika jana alisema kuwa wametoa muda mrefu ili waandaliwe vifaa vya upigaji kura kwa uhakika.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete alisema kuwa muda huo ni mrefu sana kwani maeneo mengine yalifanya uchaguzi kesho yake. "Nadhani suala la siku ya kupiga kura lirudishwe nyuma kwani Ijumaa ni mbali sana hivyo kuna haja ya wahusika kuliangalia hilo ili wasipishane na wengine," alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alishauri zoezi la namna ya kupiga kura washirikishwe zaidi wananchi kwani wale wanaowachagua ni viongozi wao hivyo wao ndiyo wenye nafasi kubwa ya kushauri na si viongozi wa vyama vya siasa.
Baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vilifanya uchaguzi wao jana Jumatatu badala ya Jumapili ni Kijiji cha Changarikwa, Vitongoji vya Kwamkula, Mkambala A na B, Kwaluguru A na B, Pugwe, Migola na Kwadivumo kwenye kata ya Mbwewe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Ibrahim Matovu alipoulizwa juu ya baadhi ya maeneo kushindwa kupiga kura alisema kuwa bado hajapata takwimu sahihi ndiyo anafuatilia kujua changamoto hizo.
Uchuguzi mdogo uliofanywa na mwandishi wa habari hizi ulibaini zoezi la upigaji kura ulikumbwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa vifaa vya upigaji kura kama vile upungufu wa karatasi, picha za wagombea kuwekwa kwenye nembo ya chama kisichohusika na kukosekana kwa fomu za wagombea wa nafasi ya ujumbe.