Katika jitihada za kupambana na hujuma zinafanywa mara kwa mara na baadhi ya wafanyabiasha nchini, serikali imeanza mipango ya kujenga kiwanda cha kuzalisha sukari mkoani Kigoma.
Wakati serikali ikiwa katika mipango hiyo, imesema hakuna uhaba wa sukari nchini na kueleza sukari ipo ya kutosha.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitolea ufafanuzi wa sakata linaloendelea nchini kuhusu kupanda kwa bei ya sukari, kunakodaiwa kumesababishwa na uhaba wa bidhaa hiyo.
''Hakuna crisis (tatizo) ya sukari kwa sasa. Tunataka kuidhibiti sukari inayotoka nje, kuna watu wajanja wajanja ambao walikuwa wanapata ruzuku kwenye kuagiza sukari kutoka nje. Sasa serikali tunajenga kiwanda Kigoma," alisema Mwijage.
Alisema endapo atabaini kuwa ghala lolote ambalo limefungia sukari atalichukulia hatua ya kulifunga kwa kuwa haogopi mtu yeyote katika kuchukua uamuzi.
Alisema kiwanda kitakachojengwa Kigoma, kitakuwa kinazalisha tani nyingi pamoja na kuajiri vijana wengi. Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa sukari unakuwa wa kuridhisha na hakuna uhaba wowote wa sukari.
Wakati huo huo, Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), imezishukia kampuni tatu zinazojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa sukari nchini na kuzitaka kuondoa sukari katika maghala yao mara moja na kuipeleka sokoni.
Mrugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Henry Semwaza, alisema kampuni ya Alneem Enterprise ya jijini Dar es Salaam imeficha tani 8,600 z sukari katika magodauni yake, hivyo na kutakiwa kuondoa.
Alisema kampuni ya Sukari ya Kilombero nayo imetakiwa kuwaagiza wafanyabiashara waliolipia sukari iliyozalisha kuiingiza sokoni haraka badala ya kuendelea kuihifadhi katika maghala.
Alisema kampuni ya sukari ya TPC nayo inatakiwa kuuza sukari yake yote iliyohifadhiwa katika maghala na inayoendelea kuzalishwa.
Alisema kiasi cha sukari ya akiba iliyoko nchini ni tani 12,000 na kwamba bei ya sukari inayotakiwa kuuziwa katika maduka kwa bei ya jumla ni Sh. 87,000 hadi 90,000 kwa mfuko wa kilo 50 na Sh. 2,000 hadi 2,200 kwa bei ya rejareja kwa kilomoja.
Alisema kiasi hicho cha sukari kinatosha kutumika hadi msimu mpya wa mavuno ambao unaanzia mwezi Mei.