Serikali imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuacha mara moja tabia ya kukata umeme bila sababu ya msingi. Agizo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na Naibu wake, Dkt Medard Kalemani walipofanya ziara ya kushtukiza kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo.
Mara tu baada ya kuapishwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Naibu wake, Dkt Medard Kalemani walifanya ziara hiyo ya kushtukiza kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuzungumza na Menejimenti ya Shirika hilo.
Profesa Muhongo alisema wananchi wamechoshwa na tabia ya shirika hilo ya kukatakata umeme bila kuwepo na sababu ya msingi ya kufanya hivyo.
"Haiwezekani kila mwaka matatizo ni yaleyale na nyie bado mpo ofisini, hili halikubaliki na halivumiliki. Ninataka tutengeneze historia ya kutatua matatizo ya umeme nchini. Umeme ukiendelea kukatikakatika lazima muondoke," alisema Profesa Muhongo.
Alisema wananchi wanahitaji umeme wa bei nafuu ili waweze kujikwamua na umasikini huku akieleza kwamba ni wakati mwafaka suala hilo likatazamwa kwani bei ya huduma ya umeme ikishuka bidhaa nyingine pia zitashuka.
Mbali na hilo, Profesa Muhongo aliwataka watendaji hao kujieleza ni kwanini umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuwataka waeleze wao kama Menejimenti ya Shirika hilo ni hatua zipi ambazo tayari wamezichukua kuhakikisha hali hiyo haijirudii.
Alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuifanya Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na hivyo inatakiwa kuwa na umeme wa uhakika. Vilevile aliwataka waeleze ni kwa nini huwa wanachelewa kufika maeneo ambayo kumetokea hitilafu hali yakuwa wananchi wanatoa taarifa mara tu wanavyoona hitilafu husika.
"Huduma zenu haziridhishi, unakuta transfoma imeharibika ama nguzo imeanguka na taarifa mnaletewa niambieni ni kwanini huwa hamfiki kwa wakati," alihoji Profesa Muhongo huku akiwasisitiza wabadilike. Profesa Muhongo alisema tangu ametangazwa amepokea simu nyingi kutoka kwa Watanzania wakisikitishwa na hali ya umeme nchini.
"Nimepokea simu kwa wananchi wa mikoa mbalimbali nchini hususan Arusha na Mwanza wakinilalamikia kuhusu kukosekana kwa huduma ya umeme kwenye mikoa hiyo. Nataka leo hii mnipe jibu tatizo ni nini," alihoji Profesa Muhongo.
Alisema ni wakati sasa viongozi hao wawe wabunifu vinginevyo Serikali haiwezi kuwaelewa kwani kila kukicha tatizo la umeme linaonekana kuendelea kuwa palepale. "Kwa miaka yote mliyofanya kazi hapa Tanesco naona mmeshindwa kubuni mbinu zitakazolipeleka shirika kule ambapo wananchi wanataka. Ninawaagiza kujitathmini kama kweli mnafaa kuendelea na majukumu yenu," alisema Muhongo.
Alisema wananchi wamechoka kusikiliza maneno bila kuona vitendo na hivyo kuwaagiza kuhakikisha wanabadilika haraka iwezekanavyo kabla Serikali haijachukua hatua zingine. Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Waziri wa wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alisema kazi kubwa ya shirika hilo ni kuwapelekea wananchi huduma ya umeme na si vinginevyo. Alisema ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imebainisha lengo la Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapelekewa huduma ya umeme na sio ahadi na maneno yasiyokuwa na tija. Aliwaagiza kuhakikisha katika utendaji wao wanazingatia masuala makuu manne ambayo aliyaelezea kuwa ni maadili, uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia taaluma badala ya kufanya kazi kwa mazoea. Akizungumzia suala la wizi wa umeme, Dkt Kalemani alisema watumishi wasio waadilifu wa shirika hilo nao wanahusika kwa namna moja ama nyingine na hivyo kuwaagiza watendaji hao kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa mapema iwezekanavyo.
"Tubadilike, tutafsiri mipango yetu kwa vitendo, tupange na tutekeleze. Hakuna muda wa kuendelea kuzungumza mipango bila utekelezaji. Wananchi wanahitaji kuona utekelezaji unafanyika," alisema. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba aliwapongeza viongozi hao kwa kuteuliwa kwao na kuahidi kuendeleza ushirikiano ili kutatua changamoto mbalimbali. "Tumefurahi na uteuzi huu kwani mnaielewa vizuri sekta hii ya nishati; tupo tayari kufanya kazi na tunawahakikishia kuzingatia maagizo yenu bila kuchelewa," alisema Mramba.
Baada ya kuzungumza na menejimenti ya shirika hilo, Waziri Profesa Muhongo alisema kesho atasafiri kuelekea katika Bwawa la Hale ili kujionea hali ilivyo ikiwa ni pamoja na kuzungumza na Watendaji walioko katika maeneo hayo na huku Naibu wake akikutana na taasisi pamoja na makampuni mbalimbali yanayohusika na sekta ya nishati nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Makao Makuu ya TANESCO. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akisisitiza jambo wakati wa kikao chake cha kushtukiza na Menejimenti ya TANESCO. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo.