Wednesday, December 30, 2015

DART yaonya madereva wazembe



DART yaonya madereva wazembe
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kuanza jijini Dar es Salaam, baadhi ya madereva wasio makini wameanza kuharibu miundombinu ya mradi huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa jiji hilo.

Uharibifu wa hivi karibuni kabisa kutokea unahusu basi lenye usajili T430 (YUTONG) ikiendeshwa na Abuu Nassar mali ya Kampuni ya Fashion Tourism Investment Limited kugonga Kituo cha Kimara Baruti na kusababisha uharibifu.

Meneja Msimamizi wa Miundombinu wa wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi Mohamed Kuganda amewaambia waandishi wa habari jana kuwa uharibifu huo ulitokea tarehe 26 usiku mwezi huu.

"Ni jambo la kusikitisha kwamba hili limetokea siku chache tu kabla ya kuanza kwa huduma hii ya usafiri," alisema Bw. Kuganda.

Basi hilo lilikamatwa na dereva wake yuko chini ya ulinzi akisubiri hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.

Ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo kupita katika barabara ya mradi kwa mwendo wa kasi na kisha kuacha njia na kugonga kituo hicho.

Ni kosa kwa gari lolote kupita katika barabara ya mradi.

Kwa mujibu wa Kuganda, TANROADS imeiagiza kampuni ya SMEC kufanya tathmini ya uharibifu uliojitokeza ambapo kampuni inayomiliki basi hilo itawajibika.

Aliwataka madereva kuzingatia sheria za barabarani na kusoma vibao vinavyoelekeza matumizi mbalimbali ya barabara ili kujiepusha na ajali.
Aliwasisitiza madereva kuendesha magari chini ya spidi 50 katika maeneo ya mradi na kusimama katika matuta.

"Ajali hii ingetokea mchana ingekuwa ni hatari kwa kuwa barabara hii inatumiwa na waenda kwa miguu wengi," alisema na kuongeza kuwa madereva wanatakiwa kuwa waangalifu na kwamba DART haitawavulilia wanaovunja sheria.

Pia aliwataka waenda kwa miguu wanapovuka barabara, wapite katika maeneo yanayotakiwa na kuwa waangalifu.