Sunday, September 13, 2015

Maofisa hawa wa Uhamiaji wanastahili pongezi


Maofisa hawa wa Uhamiaji wanastahili pongezi

SEPTEMBA 8, mwaka huu, gazeti hili lilikuwa na habari isemayo 'Maofisa wasumbufu uhamiaji waripotiwe'.
Katika habari hiyo, kilielezewa kisa cha uzembe kilichofanywa na maofisa wa kitengo cha alama za vidole katika makao makuu ya uhamiaji, waliowakimbia wateja ili kuwahi nyumbani. Kwa mujibu wa habari hiyo, wateja waliokimbiwa walikuwa wakisubiri huduma ya kuchukuliwa alama za vidole, ili waendelee na utaratibu mwingine wa kupata hati hizo za kusafiria.


Bila kujali kuwa wateja hao walikuwa miongoni mwa watu waliofika katika ofisi hizo mapema kabla ya muda wa mwisho wa kupokea wageni kwenye ofisi hizo kufika, yaani saa 8:00 mchana, waliamua kubeba mikoba yao na kuondoka wakidai kuwa muda wa wao wa kufanyakazi kwa siku hiyo ulikuwa umekwisha.
Kama haitoshi, mmoja wao aliyeona uwepo wa wateja wale ni usumbufu kwake, aliamua kuwadanganya waelekee kwenye ofisi ya jirani ya kuchukua alama za vidole, akidai kuwa mhusika aliyekuwa katika ofisi ile ndiye aliyekuwa anatakiwa kuwachukua alama hizo za vidole wakati ule.
Jambo la kushangaza mfanyakazi huyo aliyeondoka aliwaelekeza watu kwenda kwa kiongozi wake, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Hati za kusafiria, mwenye cheo cha Naibu Kamishna wa Uhamiaji, aitwaye Crispin Ngonyani.
Inaelezwa kuwa, baadhi ya wateja walioamini walichoambiwa na ofisa yule, walitekeleza maelekezo yake na kufoleni nje ya ofisi ya Ngonyani aliyekuwa 'bize' akiwajibika kwa kazi zake za kila siku. Hata hivyo, kutokana na maelezo ya habari hiyo, Naibu Kamishna huyo hakusita kuwakaribisha waliokuwa wakisubiri kumwona na kuwasikiliza.
Kutokana na habari hiyo, ilielezwa kuwa, baada ya kugundua uzembe uliofanywa na maofisa hao, hususan tabia ya kuudhi iliyooneshwa na ofisa aliyewakimbia wateja na kisha kuwadanganya wahamie kwa mkuu huyo kuchukuliwa alama hizo, huku akijua kuwa ilikuwa ni kazi yake, aliamua kuziba pengo hilo la uzembe kwa kuhakikisha wateja waliovuta subira hadi wakati huo wanahudumiwa.
Inawezekana ni kwa sababu ya kufahamu uzembe uliofanywa na maofisa hao, Ngonyani anaelezwa kuamua kumwomba ofisa mwingine mwenye cheo, aitwaye Pilly afanye kazi ya kuchukua alama za vidole. Kwa kuwa Pilly alifanikisha hilo, aliweza kuwafanya wateja husika watoke wakiwa na amani na furaha, wakijua kuwa siku ile haikupotea bure.
Hata hivyo, baada ya kuzungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili kuhusu kadhia hiyo, Ngonyani aliwaomba watanzania wanaofuata pasi za kusafiria wasiwe waoga kuwaripoti kwa uongozi wa uhamiaji maofisa wote wanaoendekeza uzembe.
Alisema, wateja watumie namba zilizobandikwa kwenye madirisha ambako wanakwenda kuhudumiwa, ili hatua dhidi yao zichukuliwe na huduma ziboreshwe. Kwa mtazamo wangu, hiyo ni hatua nzuri ya kuboresha huduma inayopaswa kuigwa na ofisi nyingine zenye dhamana ya kuhudumia umma, za serikali na binafsi pia.
Aidha, kutokana na hatua iliyochukuliwa na Ngonyani 'kuziba pengo' la uzembe ule, ninapenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa sababu alifanya hivyo kuhakikisha imani ya wateja kwa ofisi ya umahiaji inaendelea kuwepo, licha ya kilichotokea.
Pongezi Ngonyani, pongezi Pilly. Endapo maofisa hawa wangeamua kuwa 'wabaya' kwa wateja, wangeamua kuwaambia waondoke na kurudi kesho kama walivyofanya waliokuwa wakiwahi nyumbani.
Mbali na maofisa viongozi hao, ninapenda kumpongeza Naibu Kamishna mwingine wa Uhamiaji katika makao makuu hayo, Bashir Mang'enya wa kitengo hicho cha pasipoti, kwa kujitoa kwake kuhakikisha wateja wanaokuwa wamejaa kwenye ofisi hizo wanahudumiwa ipasavyo.
Ni kweli kwamba mtu yeyote anaweza kusema kuwa wanachokifanya maofisa hao ni kutimiza wajibu wao, sikatai lakini tujiulize, katika mazingira ya kuwepo maofisa wakimbilia nyumbani kama wale, wakijitokeza wachache wanaojituma hawastahili kupongezwa? Chonde maofisa wa taasisi za serikali msiofanya kazi kwa wito, msisababishe taasisi zenu zionekane hazifai kwa uzembe wenu

HABARI LEO.