Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameanzisha staili mpya ya kampeni kwa kuwaruhusu wananchi kuuliza maswali ya papo kwa papo.
Staili hiyo aliianza jana katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kijiji cha Mvumi Jimbo la Mtera, wilayani Chamwino mkoani Dodoma hatua inayolenga kujua kero zinazowakabili ili akipewa ridhaa ya kuiingia ikulu aweze kuzipatia ufumbuzi.
Mkazi wa kijiji hicho, Maiko Makangi, alikuwa wa kwanza kupewa nafasi ya kuuliza kwa kumtaka Lowassa aeleze alipokuwa waziri mkuu alijenga hospitali ngani katika nchi nzima.
Makangi pia alimuuliza Lowassa inakuwaje anautaka urais wakati anatuhumiwa na kashfa ya Richmond na
ameshughulikiaje nyumbani kwake mkoa wa Arusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo imesababisha wafugaji wa mkoa huo kuwakataa watu kutoka mikoa mingine.
Hata hivyo, mgombea huyo aliyapuuza maswali ya mwisho na kujibu swali la hospitali ambalo alisema amejitahidi kujenga hospitali katika kila kata wakati alipokuwa waziri mkuu.
Naye Daniel Makabali, alimuuliza Lowassa kuwa amekaa muda mrefu madarakani alilifanyia nini jimbo la Mtera na sasa anataka kuwaomba wananchi wamchague kuwa rais.
Akijibu swali hilo alisema amefika mara kadhaa katika jimbo hilo na yapo mambo mengi aliyoyafanya wakati akiwa waziri mkuu.
Lowassa aliwaeleza wananchi hao kuwa kama watampa ridhaa, kipaumbele chake cha kwanza, pili na tatu kitakuwa ni elimu na itakuwa bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Tofauti na mikutano mingine ya kampeni iliyofanywa na mgombea huyo, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mvumi hawakuwa katika hali ya utulivu kwa kelele walizokuwa wakipiga.
WANANCHI WAZOMEA
Wakati Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akimnadi mgombea ubunge Jimbo la Mtera, Christopher Nyamwanji, baadhi ya wananchi walikuwa wakizomea hali iliyosababisha mkutano huo kutokuwa na
utulivu.
Wananchi hao waliokuwa na msimamo tofauti wakisema hawamtaki mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo ingawa hawakueleza sababu za kumkataa.
CCM WAKIPATA ASILIMIA 20 WANABAHATI
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, akizungumza katika mkutano huo alisema mikoa mingine kama CCM itapata asilimia 20 itakuwa bahati kwasababu wananchi wamechoka kutokana na kukosa dawa katika hospitali,
watoto wao kukaa chini na wanawake kukosa huduma wanapojifungua.
"Watoto wetu walikuwa wanakaa kwenye madawati leo hii wanakaa chini, elimu inazidi kushuka badala ya kuwalipa walimu vizuri ili wasaidie kuboresha elimu hawafanyi hivyo," alisema.
Alisema waliozoea kukaa CCM wanawaona wao kuondoka CCM kama wajinga bila kutambua kuwa wamefanya hivyo ili kusaidia wananchi ambao wanakabiliwa na hali ngumu kimaisha kutokana na serikali ya CCM
kushindwa kuboresha maisha yao.
Alisema CCM wanawadanganya wananchi kwamba wakichagua upinzani nchi itaingia katika vita wakati siyo kweli kwani kimsingi wanaong'ang'ania kwenye madaraka ndio watakaosabaisha kuvunjika kwa amani .
Alisema kama Ukawa itakuwa haijatekeleza mambo iliyoahidi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wananchi watakuwa huru kuchagua chama kingine.
Alisema inashangaza kwa mtu kama Jaji Joseph Warioba aliyewahi kuwa waziri mkuu kudai kuwa wanachama wa CCM waliokwenda upinzani wamepungukiwa wakati wametumia haki yao ya kidemokrasia kuhama CCM baada ya kuona chama hicho hakiwezi kufanya mabadiliko ya kuwaletea wananchi maendeleo.
CHANZO: NIPASHE