MUIMBAJI mahiri wa muziki wa Injili Tanzania anayeshika kasi katika anga la muziki huo Afrika Mashariki na Kati, Upendo Kilahiro anatarajia kumsindikiza mwenzake Bonny Mwaitege anayetarajia kuzindua albamu tatu mfululizo, uzinduzi unaotarajia kufanyika Agosti 2.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, Kilahiro ataungana na Kwaya ya Wakorintho wa pili ya Mufindi mkoani Iringa.
Msama alisema Kwaya hiyo ni mojawapo ya watakaomsindikiza mwimbaji huyo kwa sababu hivi sasa sambamba na Kilahiro.
"Uzinduzi wa albamu tatu za Bonny Mwaitege unatakiwa kufanyika kwa maandalizi ya hali ya juu ambayo yanafanyika kwa mfumo wa kisasa," alisema Msama na kuongeza."Uzinduzi wa Mwaitege utakuwa ni wa aina yake kwa sababu maandalizi yake kwa yamefanywa kwa ustadi mkubwa hasa hatua za mwisho za rekodi ya albamu hizo inayomaliziwa jijini Mwanza na baadaye Nairobi," alisema Msama.
Msama alisema sambamba na muimbaji huyo, mikoa mbalimbali imeonesha nia ya kutaka uzinduzi wa albamu hizo. Aidha Msama alitoa wito kwa mashabiki wa muziki wa Injili Tanzania kujiandaa kupata neno la Mungu kupitia muimbaji huyo. Bonny Mwaitege anatamba na nyimbo mbalimbali kama Mama ni Mama, Mke mwema, Wakusamehe, fungua moyo wako na njoo uombewe na Yesu yupo.