Thursday, July 09, 2015

WASTAAFU KULIPWA PENSHENI KWA KADI MAALUM



WASTAAFU KULIPWA PENSHENI KWA KADI MAALUM

Wazee wanaolipwa pensheni na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanzia sasa watakuwa wakitumia kadi maalum kulipwa pensheni yao ya kila mwezi ili kuwalinda wasiibie fedha zao za mafao.


 
Hayo yalisemwa na Ofisa Operesheni wa NSSF, Joyce Mruma, kwenye Maonyesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam jana.
 
Alisema mfumo huo mpya utamwezesha mzee mstaafu kupata mafao yake ya kila mwezi kupitia mashine za kutolea fedha (ATM), Tigo pesa, M-pesa, vituo vya mauzo na mitandao mingine kwa kutumia kadi hiyo.
 
"Wazee wenye pensheni ambao ni wanachama wa NSSF hawatatembea tena na pesa mkononi. Katika mfumo wa zamani, wanachama wa NSSF wazee waliostaafu walikuwa wanalipwa mafao yao kupitia ofisi za posta hali iliyosababisha matatizo mengi kwa wazee hao, ikiwamo kuibiwa njiani na vibaka, lakini sasa tumeamua kubadilisha mfumo wa zamani na kutumia mfumo wa kisasa," alisema. 
 
Mruma alisema kuanzia sasa wazee watalipwa kupitia 'Smart Cards' ambazo zitawawezesha kupata fedha zao wakati wowote na mahali popote na hawatatembea  tena na fedha mkononi.
 
Aliongeza kuwa kadi hizo pia zitaunganishwa na mifumo ya maduka makubwa ili kuwawezesha wazee kununua vitu na huduma mbalimbali kupitia kadi zao.