Wakati mmoja mwaka jana, kulijitokeza taarifa kupitia magazeti ya kila siku kuwa wanasayansi wanaojihusisha na tafiti za kujua tiba na chanjo ya Ukimwi wameitangazia dunia kuwa hatua walioifikia wakati huo waliona ugonjwa huo 'siyo hatari tena' kwa vile walikuwa nazo silaha zote za kuweza kukabiliana nao, kwamba Ukimwi haukuwa tishio tena duniani.
Taarifa hizo zilionekana kuleta matumaini mapya ya maisha kwa watu wengi duniani endapo tu kama zingeleta mafanikio na kutoa tiba na chanjo halisi na hatimaye kumaliza janga hilo ambalo limesambaratisha famillia na binadamu wengi kote duniani.
Kwanza kabisa ni wajibu wetu kuwapongeza na kuendelea kuwapa nguvu ya kiuchumi ili waendelee na tafiti hizo kwani bado matokeo halisi yalikuwa bado hayajathibitishwa na mamlaka husika.
Watafiti hao, walitoa taarifa zao wakati wa Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi uliofanyika mjini Washington DC nchini Marekani na kuhudhuriwa na wajumbe wengi wakiwamo watunga sera, wataalamu wa afya pamoja na wadau wengine wanaopambana na ugonjwa huo kutoka karibu kila kona ya dunia hii.
Watafiti hao walisema kinachowakwamisha katika jitihada zao za utafiti ni ukosefu wa fedha. Walidai fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeleza tafiti na kuweka sera mpya za kukabiliana na Virusi Vya Ukimwi (VVU) duniani.
Jopo la wanasayansi nguli duniani wanaoendelea na mkutano huo wamekiri kuwa wamefanyia utafiti wakutosha VVU na ndiyo maana wanatamba kuwa wamefanikiwa katika kuvidhibiti.
Walidai kuwa "kwa sasa tunazo silaha zote za kisayansi kumalizia mbali hili gonjwa la Ukimwi. Kilichobaki ni kutumia kikamilifu utaalamu huu katika fursa hii tuliyonayo," alisema Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU, Dk. Elly Katabira.
Mmoja kati ya wachangiaji wa mkutano huo, Profesa Diane Havlir ambaye ni Mtaalamu wa Tiba katika Chuo Kikuu cha California alisema "Ujumbe wangu kwenu, hasa kwa watunga sera ni kwamba, endeleeni kuwekeza katika mipango ya kisayansi".
Kinachohitajika zaidi katika kufanikisha tafiti hizo ni rasilimali fedha, na ndio maana wataalamu wa tafiti hizo wameitaka jumuiya ya kimataifa kuwekeza zaidi katika tafiti wanazoendelea nazo, ili hatua za kukamilisha na kuwashirikisha wafadhili na watunga sera ziende kwa kasi na chanjo hiyo ianze kutumika mapema.
Juhudi za watafiti wa tiba na chanjo ya maradhi ya Ukimwi zilianza zaidi ya miaka 30 iliyopita, VVU kwa mara ya kwanza viligundulika mwaka 1981, na ilikuwa vigumu kupata dawa ya kuviua kwa sababu ya tabia zao na uwezo wa kujigeuza kuwa sehemu ya mwilina kutumia selikinga kuzalisha virusi wengine.
Wanasayansi hao walitoa kauli hizo za matumaini za kukabiliana na VVU mbele ya viongozi mashuhuri wa kisiasa akiwamo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton pamoja na Rais wa Ufaransa, Francoise Hollande.
Nimeona nielezee kwa ufupi sana juhudi za watafiti wanasayansi hatua waliyofikia katika jitihada za kupambana na gonjwa hilo katili ambalo hakuna binadamu duniani ambaye hajawahi kulisikia, na kwa hakika sehemu kubwa ya binadamu duniani wameshalizwa kwa kufiwa na ama jamaa, ndugu, jirani, rafiki nk. kutokana na gonjwa hilo ambalo bado mpaka sasa halijapatiwa tiba wala chanjo.
Dunia ilishakata tamaa na kudhani labda VVU vimeletwa duniani kama sehemu ya adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na wimbi la dhambi binadamu wanazozifanya kinyume na mapenzi yake.
Pamoja na taarifa hizo za watafiti, bado tunawajibika kuwa waangalifu na waoga, tunatakiwa tujipime na kujua kuwa taarifa za matokeo ya tafiti zilizotolewa kwenye mkutano huo wa Washington hazituhalalishii kuamini moja kwa moja kuwa tiba ya gonjwa hilo imeshapatikana.
Bado zipo hatua nyingi za kukamilisha mchakato wa kupitisha tiba hiyo kwa wananchi.
Kinachotakiwa ni wadau pamoja na taasisi nyingine kuwawezesha kiuchumi watafiti hao ili maeneo yaliyobakia yakamilike mapema na hatimaye mamlaka husika ziweze kutangaza na kuidhinisha kuwa tiba na chanjo dhidi ya VVU imeshapatikana.
Licha ya tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa kuna kila dalili ya kupatikana kwa chanjo, miaka michache iliyopita, waligundua moja ya dawa zinazotumika kupunguza makali ya VVU ambayo ni ARV ijulikanayo kama Truvada.
Dawa hiyo ina uwezo wa kumkinga mwathirika asimwambukize mpenzi wake wanayeshiriki naye tendo la ndoa. Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) iliidhinisha Trivada ambayo imekuwa ikitumika sehemu mbalimbali duniani tangu mwaka 2004 kuwa ni tiba ya kuzuia kuenea kwa VVU.
Kwa mujibu wa maelezo ya FDA, mwathirika anayetumia ARV anaweza kujamiiana na mwenza wake ambaye hana VVU bila kutumia kondomu bila kumwambukiza.
Inawezekana kabisa kuwa hatua waliyoifikia watafiti ni ya mwisho katika mapambano dhidi ya Ukimwi, na kwa vile kila mtu ameshaingia woga wa kuambukizwa ugonjwa huo, ni imani yangu kuwa hadhari tulizojijengea kwa miaka yote hii tangu ugonjwa huo kuingia, zitaendelea kuzingatiwa ili kujijengea heshima na maendeleo katika afya zetu.