Thursday, July 09, 2015

Mzee Kingunge atoa yake ya moyoni mjini Dodoma leo



Mzee Kingunge atoa yake ya moyoni mjini Dodoma leo
MWANASIASA mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, amekionya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutofanya dhihaka ya kumpendekeza kada yoyote kuwa mgombea wake wa urais kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, kwani kwa kufanya hivyo kitaanguka.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo Jumatano Julai 8, 2015, Kingunge ambaye ameshawahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya chama hicho alisema "ninatishwa na watu wanaotumia nguvu nyingi kwelikweli kupambana wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama, badala ya kuelekeza nguvu hizo kupambana na wapinzani wetu, hii ni hatari.', alionya

Amesema, CCM ni lazima ifuate katiba yake ili wajumbe wanaotarajiwa kutoa maamuzi watoe maamuzi sahihi na sio kupindisha katiba kwa kuanzisha utaratibu ambao sio utamaduni wa kidemokrasia.

"kuna kiongozi mmoja anasema, kada yeyote wa chama hicho aliyeomba kuteuliwa kuwania urais, endapo jina lake litakatwa hatakuwa na nafasi ya kukata rufaa, hii haijawahi kutokea na wala haipo kwenye katiba yetu.' Amesema Mzee Kingunge.
"CCM lazima imteue mtu anayekubalika ndani na nje ya chama ili chama kiweze kushinda, kinyume na hapo, hii ni njama ya kukifanya kishindwe kwenye uchaguzi".

Hivi karibuni Katibu wa Halmashauri Kuu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa hakutakuwa na nafasi ya kada wa chama hicho atakayeenguliwa kwenye mchujo kuweza kukata rufaa, kwani hakuna kanuni inayoelekeza kufanya hivyo.
Hata hivyo Kingunge amepinga kauli hiyo na kusema, inakwenda kinyume cha katiba ya CCM ambayo inaweka bayana kuwa maamuzi ya vikao vya chini yanaweza kukataliwa na vikao vya juu ikiwa ni pamoja na mwanachama ambaye anaona hakutendewa haki kuwa na nafasi ya kupinga uamuzi wa vikao vya chini.