Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya kudumu ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania) itakayofanyika leo Jumatatu, tarehe 22 Disemba, 2014 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa toka Wizara ya Sheria na Katiba, hafla hiyo itafanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi – saa 6:00 mchana katika eneo lililopo nyuma ya Jengo la Mawasiliano (Mawasiliano Towers), barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam yalipojengwa majengo hayo. Aidha, majengo haya yapo karibu kabisa na kituo kipya cha daladala cha Ubungo.
Majengo yatakayozinduliwa ni Mahakama ya Mafunzo (Teaching Court); Vyumba vya Madarasa (Lecture Theatres); Maktaba (Library); Jengo la Utawala (Administration Block); Mgahawa (Cafeteria); na Nyumba za Watumishi (Staff Quarters).
Pamoja na Makamu wa Rais, viongozi wengine watakaohudhuria ni Mawaziri, Majaji, Makatibu Wakuu, Mawakili, Wabunge, Wahadhiri na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ilianzishwa na Sheria ya Bunge (Sura 425) mwaka 2007 kufuatia jitihada na mapendekezo ya muda ya muda mrefu ya Tume na Kamati mbalimbali zilizofanya utafiti katika sekta ya sheria nchini na kuona umuhimu wa kuwa na chuo cha kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria ili kuongeza ujuzi na stadi baada ya kupata mafunzo ya nadharia katika vyuo vikuu.
Ujenzi huo wa majengo ya kudumu ya Taasisi umeigharibu Serikali zaidi ya Tshs 16.1 bilioni na ulianza mwezi Oktoba, 2010 na kukamilika mwezi Juni, 2013. Ujenzi ulifanywa na Kampuni ya BECG (Beijing Engineering Construction Group) kutoka China na ulisimamiwa na kampuni ya Co-Architecture yenye makao makuu yake hapa nchini. Kampuni hizi ndizo zilizoshinda zabuni za kazi zao.
Wanahabari kutoka vyombo vyote mnakaribishwa katika hafla hiyo.