Monday, December 22, 2014

Chuo Kikuu cha Nelson Mandela jijini Arusha chaingia mkataba na kampuni ya Huawei Tanzania


Chuo Kikuu cha Nelson Mandela jijini Arusha chaingia mkataba na kampuni ya Huawei Tanzania
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya HUAWEI Tanzania, Peter Jiang(Kushoto) na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Arusha, Profesa Lughano Kusiluka, wakisaini mkataba wa Shilingi Milioni 51 kama msaada wa kuchangia utafiti wa matatizo mbalimbali ya jamii nchini zilizotolewa na Kampuni hiyo mwishoni mwa wiki.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya HUAWEI Tanzania, Peter Jiang(Kushoto) akimkabidhi mkataba, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Arusha, Profesa Lughano Kusiluka mara baada ya kusainishana wa Shilingi Milioni 51 kama msaada wa kuchangia utafiti wa matatizo mbalimbali ya jamii nchini zilizotolewa na Kampuni ya HUAWEI mwishoni mwa wiki.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya HUAWEI Tanzania, Peter Jiang (Kushoto) na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Arusha, Profesa Lughano Kusiluka, wakiteta jambo mara baada ya kusainishana mkataba wa Shilingi Milioni 51 kama msaada wa kuchangia utafiti wa matatizo mbalimbali ya jamii nchini zilizotolewa na Kampuni ya HUAWEI Nchini mwishoni mwa wiki.

CHUO Kikuu Cha Nelson Mandela Sayansi na Teknolojia (NM-AIST) kimesaini makubaliano ya kiasi dola za kimarekani 30,000 sawa na kiasi cha shilingi hamsini na moja milioni kutoka kampuni ya Huawei Tanzania ikiwa ni katika malengo mahususi ya kuwasaidia wanafunzi wa shahada ya uzamili katika kufanya tafiti kwenye Nyanja za teknolojia na habari (TEKNOHAMA).

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo jijini Arusha mwishoni mwa wiki, Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Lughano Kusiluka amesema kuwa huu ni mwaka wa pili wa makubaliano na Huawei ya kukisaidia chuo kiasi cha dola 30,000 kila mwaka kwa muda wa miaka mitatu katika mikakati ya kuwainua wanafunzi wa Teknohama kwenye tafiti.

Profesa Kusiluka aliongezea kuwa msaada huo siyo tu utakisaidia chuo na wanafunzi kuweza kuisadia nchi yetu ya Tanzania katika kupiga hatua za kiuchumi na maendeleo kupitia sekta ya mawasiliano na habari.

"Kama mliovyomsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia wahitimu, amesisitiza kuwa tafiti za kisayansi ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa taifa lolote lile Duniani, hivyo msaada huu kutoka Huawei utaleta chachu kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi," alisema Aliongezea: "Kwa niaba ya Uongozi wa Chuo, tunaishukuru sana kampuni ya Huawei Tanzania kwa mchango wake ambao kwa kiasi kikubwa umefanikisha sana matokeo ya wahitimu hawa tulio nao leo.

Huawei wamejitolea kuchangia utafiti kwa miaka mitatu na huu ni mwaka wa pili, tunawaomba waendelee kuwa nasi hata baada ya mwaka wa tatu wa makubaliano"

Akizungumza kwa niaba ya wanavyuo wenzake waliofaidika, Michael Mollel alisema: "Binafsi natoa shukrani zangu za dhati kwa Huawei Tanzania kwa mchango huu, mimi nilifanya utafiti wangu katika jiji la Dar es Salaam, ilinichukua miezi mitatu kukamilika, na kwa gharama zilivyo katika jiji hilo, nimgekuwa katika hali ngumu sana na hata kushindwa kumaliza utafiti kama siyo kwa msaada kutoka Huawei" Mollel aliongezea kuwa mafanikio yake hadi kufikia kutunukiwa shahada ya uzamili yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na msaada huo wa Huawei waliotoa katika chuo cha NM-AIST.

Kampuni ya Huawei Tanzania mwishoni mwa wiki ilishuhudia mafanikio makubwa ya mpango wake wa kuchangia utafiti kwa wanachuo wa shahada ya uzamili katika Taasisi ya Sayansi na Technolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ya Jijini Arusha.

NM-AIST imefanya mahafali yake ya pili ambapo wahitimu wa shahada ya Uzamili walikuwa 93 na uzamivu walikuwa 13, ambayo ni asilimia 95 na karibu asilimia 50 ya jumla ya wadahiliwa wa makundi haya.

Wahitimu wa shahada ya uzamili wa kike ni asilimia 33 na wa shahada ya uzamivu ni asilimia 25. Mahafali hayo yalihudhuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dr Mohamed Gharib Bilal pamoja na waziri wa Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa.