Tuesday, July 21, 2015

JK-WATANZANIA MLIOKO NJE WASAIDIENI WENZENU


JK-WATANZANIA MLIOKO NJE WASAIDIENI WENZENU
Rais Jakaya Kikwete.

RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa nje ya nchi, kuwasaidia Watanzania wenzao wenye sifa na uwezo kuweza kujiunga na mashirika hayo ya kimataifa.


Aidha, Rais Kikwete amesema Serikali haiwadai chochote Watanzania wanaoishi nje na kufanya kazi nje ya nchi, bali kuweza kuisaidia nchi yao na ndugu zao pale inapopatikana nafasi.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipokutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi Uswisi, chini ya chama chao cha TAAS – Tanzania Association in Switzerland kwenye Hoteli ya Intercontinental mjini Geneva.
"Saidieni ndugu zenu nyumbani, lakini pia saidieni wenzenu wenye sifa ya kuweza kupata kazi katika mashirika ya kimataifa. Wenzetu katika nchi nyingi za Afrika, hasa Afrika Magharibi wanafanya hivyo, ndio maana wamejaa katika mashirika hayo ya kimataifa. Sisi tuna haya na hatufanyi hivyo," alisema Rais Kikwete.
Kuhusu matarajio ya Serikali kwa Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake haiwadai chochote. "Sisi hatuwadai chochote.
Nyie endeleeni kufanya kazi nje na kujenga maisha yenu, kazi ya maendeleo ya nchi mtuachie sisi, tunaiweza. Ushauri wangu ni wasaidieni ndugu zenu nyumbani. Dola 100 ya Marekani kila mwezi zina uwezo wa kusomesha mtoto shule."
Baada ya mazungumzo na Watanzania hao, Rais Kikwete aliwafuturisha Watanzania hao, ikiwa ni futari ya mwisho kwa Rais Kikwete na Watanzania, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Kikwete alikuwa huko kikazi, akiongoza vikao vya Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani, wanaotafuta njia za kuiwezesha dunia kujiandaa vizuri kwa majanga ya magonjwa ya kuambukiza. Raundi ya pili ya mikutano hiyo imemalizika na Rais Kikwete amesharejea nchini.