Thursday, July 30, 2015

Chenge kuhojiwa Escrow wiki ijayo.



Chenge kuhojiwa Escrow wiki ijayo.
Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge.

Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Agosti 06, mwaka huu, litamhoji Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (pichani), ambaye alikwepa mkono wa Baraza hilo Februari, mwaka huu.
 
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kwa Umma, ambao ndiyo walimshitaki Mbunge huyo, Hassan Mayunga, alisema mahojiano hayo yatafanyika chini ya Mwenyekiti wa Baraza, Jaji Mstaafu, Hamis Msumi.
 
Chenge ni mmoja wa watuhumiwa walionufaika na mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
Chenge atahojiwa baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Juni 26, mwaka huu, kutupilia mbali kesi ya kikatiba aliyoifungua kupinga kuhojiwa na Baraza hilo.
  
Februari 25, mwaka huu, Chenge alifikishwa mbele ya Baraza hilo na alisomewa mashtaka tisa ya kudaiwa kuisababishia serikali hasara, lakini kabla ya kuhojiwa aliwasilisha pingamizi la amri ya Mahakama la kuzuia mamlaka zozote kujadili au kulifanyia kazi suala lolote linalohusu kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji kifisadi wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).