Tuesday, May 12, 2015

BUSEGA: UBOVU WA MIUNDOMBINU, UDUNI WA HOSPITALI NI KERO!


BUSEGA: UBOVU WA MIUNDOMBINU, UDUNI WA HOSPITALI NI KERO!
BUSEGA ni miongoni mwa majimbo yanayopatikana ndani ya mkoa mpya wa Simiyu. Awali, jimbo hili lilikuwa ndani ya Mkoa wa Mwanza kabla ya mgawanyo wa mikoa uliofanyika siku za hivi karibuni.
Mhe. Dk. Titus Dismas Mlengeya Kamani.
Busega ni jimbo linalowakilishwa na Mhe. Dk. Titus Dismas Mlengeya Kamani ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Kabla ya hapo, Busega iliongozwa na Mhe. Dk. Raphael Chegeni. Katika donoadonoa, gazeti hili limefanya uchunguzi wa kina jimboni humo kwa kuzungumza na wananchi kwa kile walichokieleza kero za muda mrefu.
MATATIZO SUGU
Uwazi lilipata fursa ya kudadisi kwa kina na kupata mambo ambayo kwa mujibu wa wakazi wa Busega, ni kero za muda mrefu.
"Matatizo hapa ni mengi, kila mara yamekuwa yakikosa utatuzi wa kutosha licha ya kuwa na wawakilishi ambao ni wasomi wa kiwango cha juu na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kama uwaziri (Dk. Kamani)."Wakati wa kampeni, kila mgombea alikuwa akijinadi kwa kuweka ahadi kedekede kuwa atatatua matatizo haya, lakini kwa sasa kimekuwa ni kitendawili cha muda mrefu kisichokuwa na majibu stahiki," anasema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Ludayila.
Miongoni mwa matatizo sugu yanayodaiwa kuwatesa wakazi wa jimbo hilo ni pamoja na ubovu wa miundombinu ambapo barabara nyingi hazina ubora wa kiwango kinachohitajika jambo linalosababisha usafiri kuwa mgumu kwa wakazi wa jimbo hilo.
Wakazi hao wanaoendesha maisha kwa njia za kilimo cha zao la pamba na uvuvi wa samaki, wamezidi kudai kuwa huduma ya usafiri kwa baadhi ya maeneo imekuwa ni adhabu kubwa kwani magari hayafiki kutokana na ubovu wa barabara, hivyo kulazimika kutumia usafiri wa baiskeli na kutembea umbali mrefu jambo ambalo ni hatari hasa kwa wagonjwa.
Changamoto nyingine ni vifo vya wajawazito wanaokosa huduma za afya karibu na maeneo yao ya kuishi na kwamba wakati mwingine huzidiwa na uchungu hivyo kujifungulia njiani hali ambayo pia husababisha vifo kwa kupoteza damu nyingi.
Baadhi ya wananchi wa jimbo hilo wamekiri kutegemea hospitali moja ya Mkula Mission na kuwa adhabu kali kwa wakazi waishio maeneo ya mbali na hospitali hiyo kama vijiji vya Jisesa, Ngasamo, Gwamgwenge na Mwamigongwa.
"Kwa kweli huduma ya afya bado ni changamoto kubwa sana kwetu, wawakilishi wetu wamekuwa wakiahidi kuleta utatuzi lakini imebakia kuwa ni ndoto," mmoja wa wananchi wa jimbo hilo ambaye hakupenda jina lake liwe wazi anasema.
Baada ya kusikiliza kero hizo, mwandishi wetu alifanya jitihada za kumtafuta Mhe. Dk. Kamani lakini hakupatikana.
Hata hivyo, kupitia vyanzo mbalimbali kutoka jimboni humo, mwandishi wetu alipata baadhi ya maelezo ambayo mheshimiwa huyo aliwahi kuyatoa juu ya kero hizo.
"Wakati naanza kuliwakilisha Jimbo la Busega, kero zilikuwa nyingi mno ikiwemo ya afya lakini nimekuwa nikiendelea kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake pamoja na miradi mingine yenye manufaa kwa wananchi.
"Huwezi kusema sijatenda jambo kwa hapa Busega, ujue kila mabadiliko na maendeleo hayaji kwa njia rahisi, ni hatua kwa hatua, sasa ukisikiliza maneno ya wapinzani lazima watazungumzia upungufu tu na kuyaacha mazuri yote," alikaririwa Dk. Kamani.Pamoja na maelezo hayo, Uwazi linaendelea kumtafuta Mhe. Kamani ili kupata ufafanuzi zaidi wa kero zinazowakabili wapi kura wake.