Tuesday, May 12, 2015

Mwanafunzi Ahukumiwa Jela Miaka 30 na Viboko 24 Kwa Wizi



Mwanafunzi Ahukumiwa Jela Miaka 30 na Viboko 24 Kwa Wizi

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 24, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Bukanga kwa  unyang'anyi wa kutumia silaha.
 
Joseph Marigeri (21) ambaye alidaiwa  kufanya unyang'anyi katika Kata ya Makoko Manispaa ya Musoma,alihukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Baraka Maganga.
 
Awali  Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Ally Mbogoro  alieleza kuwa mwanafunzi huyo  alitenda kosa hilo Oktoba 18 mwaka jana kwa kumvamia Shukrani Habibu na kumnyang'anya simu  ya Tecno yenye thamani ya Sh 400,000 na kutokomea nayo kusikojulikana.
 
Hakimu Maganga akisoma hukumu alisema kutokana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka na utetezi, mahakama inamtia hatiani mtuhumiwa huyo hivyo kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 24.

"Kutokana na kosa la unyang'anyi ulilolifanya, kwa mujibu wa sheria natoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela  na kuchapwa viboko 24.
 
"Utachapwa viboko  12  wakati ukiingia na 12 wakati ukitoka na unayo nafasi ya kukata rufaa,"alisema Hakimu Maganga.