Tuesday, April 21, 2015

WASAIDIZI WA SHERIA WANAVYOWEZA KUMALIZA UKATILI WA KIJINSIA



WASAIDIZI WA SHERIA WANAVYOWEZA KUMALIZA UKATILI WA KIJINSIA
Mtoto akiwa amechomwa na kitu            chenye ncha kali mgongoni. Madhara ya hatua kama hii huwa nayo            mtoto katika makuzi yake yote. Huweza kumfanya awe muoga,            mwenye kujitenga na asiyejiamini maisha yake yote.

GAUDENSIA (si jina lake halisi), kwa muda mrefu amekuwa akipigwa na mumewe ambaye ni mlevi kwa sababu zisizo na msingi kama vile kuchelewa kumfungulia mlango na sasa ana makovu karibu mwili mzima.


Mwanamke huyu ambaye amekuwa hana amani na ndoa yake, mwaka jana alifikia hatua ya kurejea nyumbani kwao, lakini wazazi wake wakamrudisha kwa mumewe wakimtaka avumilie.
Kipigo cha hivi karibuni kilimwacha Gaudensia, mkazi wa kijiji cha Nzela, Geita, akiwa hana jino moja la mbele, lakini alihofia kumfikisha mumewe polisi licha ya kushauriwa kufanya hivyo na majirani ambao wamekuwa wakikerwa na tabia hiyo ya mumewe.
Lakini mwanamke huyu angekuwa akiishi Magu mkoani Mwanza angepata ushauri sahihi kutoka kwa Wasaidizi wa sheria (Magu Paralegal Unity-MAPAU) na pengine angekuwa ameshatatua tatizo hili linalomfanya asifurahie maisha ya ndoa yake.
Wasaidizi hao wa kisheria wilayani Magu wamedhihirisha kuwa msaada mkubwa kwa watu wanaokumbwa na matatizo ya ukatili kama Gaudensia kiasi kwamba bila wao matatizo yao yangeendelea kuwa siri.
Wasaidizi hao wa kisheria 25 kupitia Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto wa kike, Kivulini, walipatiwa mafunzo na mwaka mmoja uliopita na kuanza kutoa huduma hiyo kwa jamii.
Katika kipindi hicho kifupi cha utendaji kazi wa kesi 485 kati ya 525 za ukatili wa kijinsia zimepokewa na kutolewa uamuzi, mbali na wao wenyewe kutoa nasaha muhimu kwa watu kama mume wa Gaudansia.
Akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika katika kijiji cha Ihayabuyaga, kata ya Bukandwe, Mwenyekiti wa Wasaidizi wa kisheria, George Msoga, anasema kati ya kesi hizo zilizopokewa, 40 zilipewa rufaa ya kupelekwa mahakamani kwa ajili ya uamuzi zaidi wa kisheria.
Anasema kuna wanawake wengi wilayani hapo ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia na watu mbalimbali wakiwemo waume zao, lakini wamekuwa hawatoi taarifa kwa vyombo husika ili waweze kusaidiwa.
Anasema wengi wanashindwa kutoa taarifa kwa kutofahamu kuwepo kwa watu ambao wanaweza wakawasaidia na kukomesha vitendo vya kikatili vinavyoendelea katika maeneo wanayoishi.
Anasema wanasheria wasaidizi wanapopata taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya ukatili mahala, wamekuwa wakifuatilia na kutoa ushauri ambapo tayari wametoa elimu kwa kuvifikia vikundi 58 vyenye watu 1,740 juu ya ukatili wa kijinsia na hatua wanazoweza kuzichukua mara wanapokutana na hali hiyo.
Msoga anasema mbali na kupata mafanikio katika kipindi cha muda mfupi tangu wasajiliwe Septemba, 2013, yakiwemo ya kupata elimu ya usaidizi wa kisheria kwa awamu tano na kusuluhisha kesi za migogoro mbalimbali, pia wanakabiliwa na changamoto.
Changamoto hizo anasema ni pamoja na ukosefu wa usafiri wa kuwawezesha kuwafikia wanajamii kwenye vitongoji, vijiji na shule, na kukosa wafadhili mbali na ule wa Shirika la Kivulini kwani umoja wao ni wa kudumu.
Changamoto hizo anasema zinaufanya umoja huo kutoa kilio chao kwa Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kuiomba kuingiza kwenye bajeti suala la wao kupatiwa usafiri ili kuleta ufanisi zaidi ndani ya jamii na kuvumbua zaidi vitendo vya kikatili vinavyofanyika katika jamii.
Baadhi ya wanawake waliohojiwa katika maadhimisho hayo walisema matukio ya ukatili wilayani hapo yamekuwa yakipungua kwa wanawake watu wazima na kuongezeka kwa watoto kutokana na pale mwanamke anapodai haki, wanaume kuamua kutelekeza familia zao.
Utelekezaji huo wa familia wanasema humpa wakati mgumu mwanamke pale anapolea watoto peke yake na wakati mwingine kukosa uwezo wa kusomesha.
Wanasema huo ni ukatili unaowakumba watoto wengi na kusababisha watoto wa kike kwenda kufanya kazi za nyumbani wakiwa na umri mdogo ambako wengine hukutana na ukatili wa kingono na kupata mimba za utotoni.
Leticia Laurent, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Ihayabuyaga anasema wakati dunia nzima ikiangalia mchango wa mwanamke kama chachu ya mabadiliko, bado kuna kilio kikubwa miongoni mwa wanawake wanaopata nafasi ya kutoa michango yao ya mawazo juu ya siku ya wanawake.
Licha ya kaulimbiu ya mwaka huu kusema, 'Uwezeshaji wanawake, tekeleza wakati ni sasa' bado kuna mambo mengi hayaendi sawa ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, kutopata elimu bora na afya, ajira, udhalilishaji kwa wanawake na watoto wa kike kwenye familia, mashuleni, ukeketaji na rushwa ya ngono.
Anasema ipo haja ya kubadili mifumo ya kiutamaduni na mitazamo, kufanya juhudi za makusudi kuwakomboa wanamke kimawazo ili wajitambue kwamba ni sehemu muhimu katika jamii.
Katika maadhimisho hayo ambayo Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, alikuwa mgeni rasmi, Leticia anasema, watoto wengi wa kike wanaofanya kazi majumbani hufanyiwa vitendo vya kikatili na kwa bahati mbaya vitendo hivyo mara nyingi hufanywa na wanawake.
"Kuna shuhuda ambazo zimekuwa zikitolewa na watu mbalimbali zinazowahusisha wanawake kufanya vitendo hivyo vya kikatili ikiwemo kuchomwa mikono moto, kufanyishwa kazi ngumu kuliko umri wake na kukatishwa masomo kwa ajili ya kuajiriwa kazi za ndani," anasema.
Anasema tatizo la mimba za utoto hujitokeza pale watoto wa kike wanapomaliza shule na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari na hata kwa wale wanaoendelea na elimu ya sekondari kutokana na sekondari hizo kuwa mbali na makazi.
Mtoto wa kike anakuwa kwenye hatari kubwa hata kama atapata nafasi ya kuendelea na masomo kutokana na kutembea umbali mrefu wa kwenda na kurudi hivyo kuwepo na hatari ya kubakwa njiani ama kurubuniwa na wanaume wasio na upeo.
Katika hotuba yake, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo katika maadhimisho hayo anasema Serikali ya mkoa wa Mwanza imeweka mkatati wa kuondoa hali ya ubaguzi wa aina zote katika jamii.
Katika hotuba hiyo iliyosomwa na Ndaro Kulwijira aliyemwakilisha katika maadhimisho hayo, Mulongo anasema sera ya elimu inahakikisha kuwa wasichana wanapata nafasi sawa ya kuingia katika mfumo rasmi wa elimu ili kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
"Serikali inafanya juhudi kubwa katika kutoa elimu bila ubaguzi wa kijinsia kwani kumekuwepo na ongezeko katika uandikishaji wanafunzi katika ngazi zote lakini kiwango cha ufaulu na kuendelea na elimu ya juu kwa wasichana kipo chini," anasema.
Hali hiyo anasema inasababishwa na sababu mbalimbali zikiwemo za wasichana kukosa muda wa kutosha wa kujisomea, hivyo ni muhimu kujenga mabweni ya kutosha kwenye sekondari za kata ili wapate muda wa kutosha wa kujisomea.
Mkuu huyo wa mkoa anawasisitiza wazazi na walezi kuwajibika kuwafundisha watoto wa kike na wa kiume maadili mema huku akiyataka mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi kushiriki katika kutetea na kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya jitihada za kuhakikisha wanawake wanachukua angalau nusu ya nafasi zilizopo kwenye vyombo vya maamuzi ambapo kati ya wabunge 348 wanawake ni 125 wakiwemo 21 wa majimbo na 101 wa viti maalumu.
Kundi la wanawake lina mchango mkubwa katika jamii hivyo linapasa kuhamasishwa na kuelimishwa zaidi kwa kupewa vikundi kama hivyo vya wasaidizi wa sheria ili kusimamia haki zao za msingi.

HABARI LEO