Saturday, April 04, 2015

Hali ni tete: Nyaraka za umiliki wa Zanzibar kutoka kwa wajerumani zaibwa na ofisa wa ubalozi wa Oman



Hali ni tete: Nyaraka za umiliki wa Zanzibar kutoka kwa wajerumani zaibwa na ofisa wa ubalozi wa oman


Nyaraka za kale za mikataba ya kimataifa ya Zanzibar na Ujerumani, inayohusu umiliki wa Zanzibar katika eneo la mwambao wa Pwani ya Afrika ya Mashariki kuanzia Mombasa hadi Kilwa, zimeibwa katika Nyumba ya Nyaraka Kilimani.
  
Nyaraka hizo zinadaiwa kuibwa na ofisa mmoja wa Ubalozi wa Oman kwa utashi wake na si kwa amri ya Serikali ya Oman, kama ilivyodhaniwa na baadhi ya watu.
  
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, ambalo limekuwa likiandikwa kwa mtazamo tofauti, kiasi cha kupoteza ukweli wake.
  
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipokea ripoti ya wizi wa nyaraka, iliyowasilishwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahmoud Mohamed Mussa (CCM), ambayo ilimtaja Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi  Mdogo wa Oman, Zanzibar, Humud, kuhusika na tukio hilo kwa kurubuni wafanyakazi wa ofisi ya nyaraka.
  
Taarifa hiyo ilisema wizi wa nyaraka, ulifanyika katika nyakati tofauti kwa kuwahusisha wafanyakazi hao, ambao walikuwa wakishirikiana na karibu na ofisa mwandamizi wa ubalozi mdogo wa Oman uliopo Zanzibar.
  
Kutokana na taarifa hiyo, Aboud alisema wizi wa nyaraka mbalimbali za kale, uliofanywa katika nyumba ya nyaraka iliyopo Kilimani, ulifanywa kwa utashi wa ofisa mmoja wa ubalozi huo na sio kwa maelekezo ya Serikali ya Oman.
  
Alisema wizi huo kwa kiasi kikubwa umesababisha upungufu mkubwa wa nyaraka muhimu katika nyumba ya nyaraka Kilimani, ambazo hutumiwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa mambo ya kale na wanafunzi wa masomo ya elimu ya juu .
  
"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa ufafanuzi wa suala la upotevu wa nyaraka katika nyumba ya nyaraka Kilimani na kwamba Serikali ya Oman haihusiki na wizi huo ambao umefanywa na mtu mmoja kwa utashi wake,"alisema.
  
Alisema Serikali inafuatilia suala hilo kwa karibu zaidi ili kuhakikisha nyaraka zilizoibwa, zinarudishwa na wahusika ikiwemo baadhi ya watumishi wa Serikali, wameanza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
  
Aboud alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi, ambazo zimebahatika kuwa na nyaraka muhimu za mambo ya kale katika utawala wa Kisultani na utawala wa Uingereza na Ujerumani katika mikataba yake.
  
Alifafanua kuwa Serikali ya Oman imetoa misaada mingi kwa Zanzibar, ikiwemo ya kuimarisha majengo ya kale, makumbusho na nyaraka ili kuwepo kwa uhifadhi wa nyaraka sahihi kwa ajili ya kukuza maendeleo ya sekta ya utalii.
  
"Serikali ya Oman inatekeleza makubaliano ya kuimarisha mambo ya kale na makumbusho kwa ajili ya kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia kuimarisha utalii," alisema.