Saturday, April 04, 2015

Watanzania walioathirika mauaji ya Kenya watafutwa......Juzi Al Shabaab Walishambulia Kenya Na Kuua Watu 147



Watanzania walioathirika mauaji ya Kenya watafutwa......Juzi Al Shabaab Walishambulia Kenya Na Kuua Watu 147
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, unafuatilia kama kuna wanafunzi wa Tanzania waliojeruhiwa au kuuawa katika shambulio la kigaidi, lililoua wanafunzi 147 wa Chuo Kikuu nchini humo.
  
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Membe alisema ubalozi huo unatarajiwa kumpa taarifa mapema iwezekanavyo na leo atatoa taarifa kuhusu mauaji hayo, yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab.
  
"Kuhusu suala hilo nitatoa taarifa kesho (leo) baada ya kupata taarifa rasmi kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini humo….na nitajua nitatoa kwa kuita waandishi au kutuma taarifa tu," alisema Membe aliyekuwa akitoka katika Misa ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph.
  
Alisema hajapata taarifa zozote, lakini ubalozi wa Tanzania nchini humo unaendelea kufuatilia kama kuna wanafunzi wa Kitanzania waliokuwa wakisoma chuoni hapo na kufa au kujeruhiwa.
  
Chuo kikuu hicho nchini Kenya kililipuliwa na magaidi wa kundi la Al-Shabaab na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa huku baadhi ya wanafunzi hawajulikani walipo.