Kahama
WAKAZI wa Kijiji cha Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, jana walilazimika kufukua makaburi mawili walimokuwa wamezika watoto watano wa familia moja waliofariki dunia juzi baada ya mvua kubwa ya mawe kunyesha kijijini hapo.
Ufukuaji wa kaburi hilo ulifanyika mchana na kuitoa miili ya watoto hao, Luku Masemba (14), Paschal Masemba (11), Mulyante Masemba (9), Sesela Masemba (7) na Masele Masemba (5).
Taarifa zilizopatikana zinasema kuwa kaburi hilo lilifukuliwa baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kuagiza lifukuliwe ili marehemu hao wazikwe kila mmoja katika kaburi lake.
Kabla ya agizo hilo lililotolewa na Mpesya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, miili ya watoto watatu wote wa kike ilikuwa imezikwa katika kaburi moja.
Wakati watoto hao wa kike walikuwa wamezikwa katika kaburi moja, maiti mbili za watoto wa kiume zilikuwa zimezikwa katika kaburi moja.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, maiti hizo zilikuwa zimefungwa kwenye mifuko ya sandarusi baada ya wananchi kukosa sanda kutokana na Serikali kuchelewa kutoa utaratibu wa namna ya kuzikwa miili hiyo.
"Nimeambiwa mmewazika hawa watoto watatu kaburi moja na wengine kaburi lao moja. Hapana, hapana, huu siyo utaratibu hata kidogo.
"Nataka hawa marehemu wafukuliwe na kila mmoja azikwe kwenye kaburi lake siyo kama mlivyofanya ninyi.
"Suala la kuzikwa watu kwa pamoja labda itokee hawatambuliki na ndugu zao hawajajitokeza.
"Hawa watoto ni wa familia moja na mnawafahamu kwa majina na umri wao, iweje muwazike kaburi moja watatu na jingine wawili?
"Naagiza wafukuliwe na wazikwe upya katika mazingira ya binadamu," alisema Mpesya.
Familia nyingine iliyopoteza watu watano kufuatia mafuriko hayo ni ya Donald Lubunda iliyo umbali wa kilomita moja kutoka mahali ilipo familia ya watoto hao watano.
Mahitaji ya msaada
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwakata, Shaban Jumanne, alisema zaidi ya tani 20 zinahitajika haraka kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko hayo na kwamba kati ya watu 42 waliofariki dunia, wengi wao ni watoto wa kuanzia umri wa miaka 14.
"Wakazi zaidi ya 4,370 katika kaya 456 zilizoathirika na janga hili hawana makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na kuangushwa na mvua.
"Walioathirika zaidi wanafikia watu 300 na mbuzi 86, kuku 78, ng'ombe watano, bata zaidi ya 30 na paka zaidi ya 20 wamekufa katika maafa haya," alisema kiongozi huyo wa Serikali.
Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alisema yeye binafsi ametoa msaada wa mifuko 200 ya unga yenye thamani ya Sh milioni tatu.
Alisema maafa hayo yalitanguliwa na mafuriko mengine yaliyotokea katika Kijiji cha Segese jimboni humo na kuharibu nyumba zaidi ya 55.
Pamoja na hayo, alimuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waende kijijini hapo kuwasaidia waathirika hao.
PINDA AWASILI
Kutokana na tukio hilo, jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwasili kijijini hapo na kuagiza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Kahama, kuhamishia shughuli zote za uratibu wa maafa katika kambi hiyo.
Aliagiza pia maofisa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutembelea eneo la maafa na kufanya tathmini kwa ajili ya kuiongezea nguvu Hospitali ya Wilaya ya Kahama inayohudumia waathirika.
"Watu 42 waliofariki dunia katika janga hili ni wengi sana, nataka shughuli zote za uratibu wa maafa zihamishiwe hapa kwenye kambi.
"Serikali kwa upande wake, itatoa misaada yake mikubwa na hakuna atakayekosa msaada huo maana tumejipanga vizuri," alisema Waziri Mkuu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi, aliiambia MTANZANIA kuwa hospitali yake ilizidiwa na wagonjwa na kulazimika kuomba msaada kwa hospitali za jirani.
Juzi ililiripotiwa watu 42 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 91 wamejeruhiwa vibaya baada ya mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha katika Kijiji cha Mwakata, Kata ya Isaka, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Pamoja na vifo hivyo, nyumba za makazi na majengo ya taasisi mbalimbali, yamebomolewa na mafuriko yaliyosababishwa mawe kusambaa kijiji kizima.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, aliiambia MTANZANIA kwa simu juzi kwamba zaidi ya kaya 100 zimeathiriwa na mvua hiyo, nyumba 160 zilibomolewa na zaidi ya watu 600 hawana makazi.
Kuhusu vifo vilivyotokea, Mpesya alisema kuna baadhi ya familia zilipoteza watu wote na nyingine zilipoteza baadhi ya wanafamilia.
"Kuna familia moja ilikuwa na watu saba wote wamefariki dunia, familia nyingine ilikuwa na watu watano, wote wamepoteza maisha na familia nyingine zilipoteza watu kadhaa tu," alisema Mpesya.
Katika maelezo yake, Mpesya alisema mvua ya mwisho kubwa kunyesha mkoani Shinyanga ilikuwa Septemba 4 mwaka jana ambako mabwawa ya maji katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyankulu yalifurika maji na kutiririsha maji ya kemikali katika maeneo ya makazi ya wananchi.
Wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, mtoa taarifa mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Karandi, mkazi wa Kijiji cha Mwendakulima ambaye alikwenda kijijini hapo baada ya mvua hiyo kunyesha, aliiambia MTANZANIA kwa simu juzi kwamba mifugo mbalimbali ikiwamo ng'ombe, mbuzi, kondoo, punda, kuku, nguruwe na mingine, imekufa maisha kutokana na kukumbwa na mafuriko.