Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utamaduni Bibi Leah Kihimbi akimkaribisha mgeni rasmi kufungua kikao cha kumi cha Sekta ya Utamaduni jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel na katikati ni Mkurugenzi msaidizi Lugha Bibi Shani Kitogo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel akiwasalimia wadau wa Utamaduni huku akiwa ameshika moja ya dhana za utamaduni alipokua akifungua kikao cha kumi cha Sekta ya Utamaduni jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi msaidizi Lugha Bibi Shani Kitogo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel akizungumza na wadau wa Utamaduni alipokua akifungua kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi msaidizi Lugha Bibi Shani Kitogo.
Afisa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Mbeya Bw. Godfrey Msokwa akichangia mada wakati wa kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi msaidizi Lugha Bibi Shani Kitogo.
Mmoja wa washairi (kushoto) akiburudisha wadau wa Utamaduni wakati wa kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Kikundi cha ngoma kijulikanacho kama Jivunie Sanaa Tanzania kikitumbuiza wakati wa kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel (waliokaa mwenye suti) katika picha ya pamoja na wadau wa Sekta ya Utamaduni baada ya kufungua kikao kazi cha kumi cha Sekta hiyo jana jijini Dar es Salaam. (Picha zote na: Genofeva Matemu – Maelezo)………………………………………………………………………
Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Maafisa Utamaduni na wadau wa utamaduni wametakiwa kutumia sanaa kupitia fani mbalimbali kuhamasisha juhudi za kuifahamu na kuipokea katiba inayopendekezwa ili jamii ya watanzania kuweza kujipatia katiba inayokidhi mahitaji yao.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel alipokua akifungua kikao kazi cha kumi cha Sekta ya Utamaduni, Uwanja wa Taifa jana jijini Dar es Salaam.
Profesa Gabriel amesema kuwa lengo la kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni ni kutanabaisha maudhui ya Katiba inayopendekezwa hivyo kuwataka wadau wa utamaduni kutumia tasnia ya sanaa inayoumbwa na herufi K tatu zinazolenga Kuhabarisha, Kuelimisha na Kuburudisha jamii katika masuala mbalimbali.
"Utamaduni ni kama inta inayoshikamanisha watu, ni vyema wadau wa utamaduni mkatumia talanta mliyonayo kufikia fikra za watu kwani suala la katiba pendekezwa ni letu sote kama watanzania hivyo tujivunie kwa kuweka mambo kwenye vitendo na kuishi yale tunayoyasema" amesema Profesa Gabriel.
Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utamaduni Bibi. Leah Kihimbi amesema kuwa sanaa imekua ikitumika kusaidia makundi mbalimbali katika jamii kutoa sauti zao kwenye mambo mbalimbali na kuamini kuwa sanaa ina nafasi kubwa ya kuhamasisha na kuelimisha jamii maudhui ya katiba inayopendekezwa.
Bibi. Kihindu amesema kuwa kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni kimewashirikisha maafisa utamaduni kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara kikiwa na madhumuni ya kueleza mchango wa fani za sanaa katika kuelimisha umma maudhui ya katiba inayopendekezwa na kutoa ufafanuzi wa masuala ya Sekta ya Utamaduni yaliyozingatiwa katika Katiba inayopendekezwa.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri zote Tanzania Bara, Afisa Utamaduni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Bw. Godfrey Msokwa amesema kuwa kikao kazi cha Sekta ya Utamaduni kitawawezesha wadau wa utamaduni kutumia sanaa kuifikia jamii na kutekeleza maazimio yatakayokusudiwa na kikao hicho.
Kikao kazi cha 10 cha Sekta ya Utamaduni chenye kauli mbiu isemayo Fani za Sanaa zielimishe Umma Maudhui ya Katiba Pendekezwa kimelenga kutumia sanaa kama kichocheo na mbinu mojawapo ya kuelimisha, kuonya na kuelekeza mambo mbalimbali yanayoihusu jamii.