Na Bashir Yakub.
Wapo Watanzania ambao ndoto zao ni kumiliki shule. Ninapoongelea shule simaanishi lazima yawe yale mashule makubwa. Hata shule za awali ambazo zinaanzishwa na wajasiriamali wadogo mitaani nazo ni shule kwa maana hii katika makala haya.
Nyaraka kuu inayoongoza taratibu za usajili wa shule binafsi huitwa fomu namba RS8. Huu ndio mwongozo mkuu wa usajili. Kuna mambo ya msingi na ya kisheria ambayo mtu hutakiwa kujiandaa nayo iwapo anataka kuanzisha shule binafsi.Mambo haya huwa yanakamilishwa kwa wepesi na bila usumbufu ikiwa yanapitia kwa wanasheria lakini pia mtu anaweza kufanya mwenyewe isipokuwa hata akifanya mwenyewe kuna document za lazima ambazo lazima zisainiwe na kuthibitishwa na mwanasheria.
1. USHAURI MUHIMU KWA WALIO/WANAOTAKA KUANZISHA SHULE.
Kwanza kabisa kabla ya lolote ni muhimu kujua shule yako itamilikiwa namna ipi kisheria. Utaimiliki binafsi wewe kama wewe, utaunda kampuni halafu kampuni ndo imiliki shule, au utaweka chini ya taasisi fulani. Kila kimoja katika haya kina faida zake halikadhalika hasara zake. Pamoja na hayo faida na hasara hizo zinazidiana viwango. Katika baadhi ya makala zilizopita niliwahi kuzungumza umuhimu na faida za kitaalam za kufanya biashara chini ya kampuni.Kwa ushauri wangu wa kitaalam hasa katika masuala ya makampuni nashauri kuwa ni vema sana ukianzisha mradi wa shule fungua na kampuni ili shule iwe chini ya kampuni. Zipo faida nyingi sana utazipata kupitia kufanya hivyo. Hata wenye mtaji mdogo hasa ndugu zangu wanaoanzisha nursery mitaani fungua kampuni na nursery yako iweke chini ya kampuni halafu utaona matokeo yake baada ya muda.Kufungua kampuni ni bei ndogo sana na rahisi mno hivyo si jambo la kumuogofya mtu.
2. MAOMBI YA USAJILI WA SHULE HUPELEKWA WAPI.
Maombi ya usajili wa huelekezwa kwa kamishna mkuu wa Elimu. Ofisi ya kamishna mkuu wa elimu Tanzania iko Dar es Salaam. Hata hivyo nakala ya maombi hayo hupelekwa kwa mkaguzi mkuu wa elimu wa kanda husika. Kanda husika ni kanda ambayo itaanzishwa shule husika. Mkaguzi wa kanda ndiye hujushughulikia karibia mambo yote ya msingi kuhusu usajili wa shule.
3. MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA KUJIANDAA NAYO.
Kila biashara huwa ina maandalizi yake kabla ya kuanza kwake. Shule binafsi nayo kama biashara nyingine yoyote inayo mambo ya msingi na ya kisheria ambayo mtu anatakiwa kuyazingatia kabla ya kuanzisha biashara hii.Mambo haya pia ndiyo hayohayo utayotakiwa kuyajaza kwenye fomu maalum ya kuombea usajili wa shule yako.
( a ) Jina la shule. Lazima kwanza ujue shule yako itaitwaje.Huwezi kufanya mipango ya shule bila jina. Pia jina hutakiwa kujazwa kwenye fomu maalum ya kuombea usajili.
( b ) Lazima ujue unataka kuanzisha shule ya aina gani. Shule ziko aina nyingi, unataka shule ya awali(nursery),shule ya msingi,sekondari ya form iv au v & vi. Pia ujue iwapo shule hiyo itakuwa kutwa au ya kulala, ya wasichana na wavulana au wavulana tu au wasichana tu. Kama shule yako ni sekondari lazima ujue itakuwa inashughulika na michepuo ipi sanaa, biashara,kilimo, sayansi, elimu ya ufundi au kitu gani.Haya lazima ujiandae nayo na uyajue.Pia taarifa hizi huwa zinahitajika unapokuwa unajaza fomu ya usajili hivyo ni muhmu kuziandaa.
( c ) Jambo jingine ni tarehe au kipindi ambacho shule inatarajiwa kufunguliwa. Taarifa hii hutakiwa kwasababu mamlaka za usajili zinajenga dhana(assume) kuwa mtu anapoamua kujaza fomu ya usajili basi huwa yuko tayari kuanzisha shule na hivyo lazima awe na tarehe ambayo shule yake itaanza.Hivyo lazima uandae tarehe kama una mpango huu.
( d ) Pia huwezi kuanzisha shule bila kuwa na Meneja wa Shule. Sheria inataka kabla ya usajili lazima awepo meneja na atajwe katika fomu ya usajili.
( e ) Anuani kamili ya mahali ambapo shule inakusudiwa kufunguliwa ni jambo jingine linalopaswa kufafanuliwa kupitia fomu hii. Anuani hapa si tu P.O BOX……… hapana. Unataja mtaa,kitongoji,kata,wilaya, na mkoa. Hii ndio anuani.
( e ) Anuani kamili ya mahali ambapo shule inakusudiwa kufunguliwa ni jambo jingine linalopaswa kufafanuliwa kupitia fomu hii. Anuani hapa si tu P.O BOX……… hapana. Unataja mtaa,kitongoji,kata,wilaya, na mkoa. Hii ndio anuani.
( f ) Pia uandae hati ya Umiliki wa Ardhi au Mkataba wa Pango wa eneo ambalo shule itafunguliwa.
( g )Utatakiwa kuonyesha sifa na idadi ya walimu watakaoajiriwa, uwiano wa walimu na wanafunzi kwa maana ya wastani wa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wangapi (Teacher-Students ratio)
( h ) Utatakiwa kueleza vifaa vitakavyokuwa shuleni na pia kuonyesha kiwango cha juu zaidi (maximum) cha wanafunzi wanaoweza kusoma kwa wakati mmoja katika shule itakayofunguliwa.
( I ) Kutaja kiwango cha ada unachokusudia kuwatoza wanafunzi wa shule hiyo, huku ukipambanua pia tozo nyinginezo kama vile gharama za bweni na aina ya vifaa ambavyo wanafunzi wenyewe wanapaswa kuja navyo shuleni.
4. VIAMBATANISHO MUHIMU.
Vimbatanisho muhimu vya kuandaa ni Hati za Idhini za matumizi ya Ardhi chini ya taratibu za mipango miji kutoka mamlaka husika hasa manispaa, Mhandisi wa Wilaya au Mji, serikali za vijiji, na kadhalika.
Cheti kutoka kwa bwana afya kuthibitisha kwamba eneo litakalotumika kwa ya ajili ya shule linakidhi vigezo vya afya na usalama wa wanafunzi, pia ambatanisha taarifa za wafanyakazi wasio walimu,na nakala ya ramani ya majengo.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com