Watendaji wa Halmashauri waliokaa kwenye vituo vya kazi kwa zaidi ya miaka 10, wataanza kuhamishwa wakati wowote kuanzia sasa kuleta ufanisi katika utendaji na kukomesha kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani) ameagiza ofisi za mikoa ziainishe majina ya watendaji husika, utaratibu wa kuwahamisha ufanyike kunusuru utendaji wa kazi kwenye maeneo walikokaa muda mrefu.
Alitoa agizo hilo juzi wilayani Mufindi katika mkoa wa Iringa. Alisema serikali imebaini watendaji wanaokaa kwenye vituo vya kazi kwa miaka 10 na zaidi kwenye halmashauri, wanakuwa kikwazo cha utendaji kazi wenye ufanisi kutokana na kufanya kazi kwa mazoea badala ya kitaalamu.
Alisema, "Niliwahi kwenda kutembelea halmashauri fulani nikamkuta mzee mmoja amekaa hovyo kwa kujiachia achia tu na kusahau kuwa ni mtendaji wa serikali. Ilibidi nimuulize, mzee nawe umo, akasema , ndio mheshimiwa. Nikashangaa, hata huyu! Kwa jinsi hivi alivyo atafanya kazi vizuri kweli?"
"…Nilipomwuliza nilipata majibu yaliyodhihirisha kuwa alikuwa alivyo na kutenda kazi kwa mtindo aliokuwa akiufuata kwa sababu ya mazoea yaliyotokana na kuwepo kwenye halmashauri husika kwa zaidi ya miaka 10, hii haikubaliki kwa watendaji wa halmashauri".
Pinda alisisitiza, kuwepo kituoni kwa muda mrefu kwa watendaji katika halmashauri ni miongoni mwa udhaifu unaotoa mwanya wa wizi wa fedha za halmashauri kwa sababu wanakuwa wakifahamu mbinu za kuiba na jinsi ya kukwepa kujulikana uhusika.
"Huu ni ukweli na ushahidi tumeuona katika maeneo ambako watumishi walikuwa wakiiba fedha. Kuwapangua kulisaidia sana kunusuru fedha zisiibwe katika baadhi ya halmashauri zilizokuwa na matatizo ya kifedha kutokana na wizi wakati wa kukusanya kodi na ushuru mbalimbali,"alisema Waziri Mkuu.
Katika mkutano huo, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kuandaa orodha ya watumishi wa mkoa huo waliokaa kwenye nafasi za ajira kwa zaidi ya miaka 10 na kumpelekea wafanyiwe utaratibu wa kuhamishiwa vituo vingine.
"Tafuta wote waliokaa zaidi ya miaka 10. Ni lazima tuwabadilishe... niletee orodha mapema iwezekanavyo," alisema Waziri Mkuu.
Alisema nia ya mchakato huo ni kuongeza ufanisi kwani watumishi wakikaa sehemu moja kwa muda mrefu, wanakuwa butu kwa kukosa ubunifu kwenye kazi zao, wanaota mizizi na kugeuka kuwa chanzo cha matatizo katika baadhi ya maeneo.
Wakati huo huo, ameagiza uwekwe uwiano wa idadi ya walimu katika shule zote za sekondari, kulingana na mahitaji kwa kuhamisha walimu wa ziada kutoka katika maeneo walipo sasa, kwenda kwenye maeneo yenye upungufu.
Alisema, "Kuna maeneo nimeona walimu wanakula bwerere tu kwa sababu wako wengi sana. Hawa inabidi wapunguzwe na kupelekwa kwenye shule zisizo na walimu, shushu hiyo haihitajiki kwa sababu kuna wengine wanakosa wa kuwafundisha ilhali wamelundikana eneo moja".
Jumapili wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Ipogolo, nje kidogo ya mji wa Iringa, Pinda alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Ahmed Sawa kukaa pamoja na Ofisa Elimu wake wapunguze walimu 230 waliozidi mahitaji kwenye manispaa hiyo, badala yake wawapangie kwenda vijijini.
"Manispaa inahitaji walimu 534 lakini waliopo ni 764. Hapa kuna ziada ya walimu 230 tena kwenye shule za msingi...
"Mkurugenzi kaa na Ofisa Elimu wako muwaondoe walimu waliozidi na kuwapangia waende vijijini ambako kuna mahitaji zaidi," alisema.
"Kwa upande wa shule binafsi nako pia tatizo ni lile lile. Walimu wamezidi. Mahitaji ni walimu 75 waliopo ni walimu 142 ... wanaozidi ni walimu 67," alisema Waziri Mkuu.
Aliendelea kusema, "Sina tatizo na walimu wa shule binafsi kwa sababu wao wana mfumo wao wa ajira lakini hawa wa shule za Serikali ni lazima muwaondoe tena haraka sana.
"Waondoeni waende vijijini kwenye mahitaji makubwa sababu ualimu ni ualimu tu, siyo lazima mtu awe mjini ndiyo afundishe vizuri."