Wenyeviti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutoka kushoto Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (Cuf), Dk Emmanuel Makaidi (NLD) na Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Mosena Nyambabe wakiwasili kwenye chumba cha mkutano jijini Dar es Salaam jana kuzungumza na waandishi wa habari
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umetaja mambo nane yatakayosababisha Kura ya Maoni isipigwe Aprili 30 kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete, licha ya kazi ya kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Wapigakura kuendelea mkoani Njombe.
Kazi hiyo ya uandikishaji wapigakura ambayo ni muhimu katika mchakato wa Kura ya Maoni ya kupitisha au kukataa Katiba Inayopendekezwa, imekuwa na changamoto nyingi kutokana na kutumia teknolojia ya 'Biometric Voters Registration' ambayo hukusanya taarifa za mpigakura, ikiwa ni pamoja na alama za vidole.
Ukawa, ambayo inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, pia imetaka fedha ambazo zimetengwa na Serikali kwa ajili ya Kura ya Maoni, kupelekwa kwenye uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa maelezo kuwa uboreshaji unaondelea mkoani Njombe unakabiliwa na changamoto nyingi na kutaka kura ya Maoni kuahirishwa hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo imekuja siku tatu baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuanza kuandikisha wakazi wa mji mdogo wa Makambako, ambapo kwa kasoro hizo wakazi wake wamelazimika kuiomba Nec kuongeza maofisa na vitendea kazi ili kuwezesha shughuli hiyo kukamilika ndani ya muda uliopangwa.
Viongozi wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Dk Emmanuel Makaidi (NLD) na Mosena Nyambabe (NCCR-Mageuzi), walitoa kauli hiyo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakisisitiza kuwa Serikali inalazimisha mambo isiyoyaweza.
Akitaja sababu hizo, Profesa Lipumba alisema: "Kwanza, Nec haina watumishi wa kufanya kazi ya uandikishaji. Mshauri mwelekezi kutoka Marekani aliishauri tume kuwa inahitaji kuwa na watumishi 10,000 ili kufanikisha uandikishaji nchi nzima na wapewe mafunzo ya kina ya kutumia mashine hizo."
Alisema watumishi waliopo Makambako ni wachache na wamepewa mafunzo ya siku moja tu, kabla ya kuanza kwa uandikishaji, na wengi wao hawajui kutumia kompyuta wala kamera ambazo ndiyo zinazotumika kuchukua taarifa muhimu.
Alitaja sababu ya pili kuwa ni Nec kukabiliwa na uhaba wa fedha kwa maelezo kuwa ilipewa jukumu la kuboresha Daftari la Wapigakura bila kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri na kuwapa mafunzo wafanyakazi husika sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.
"Tatu, Tume haisemi ukweli juu ya suala zima la uandikishaji. Wamesema watakamilisha kazi Aprili 28 na 30 itafanyika Kura ya Maoni. Nchi ina watu milioni 24 wenye haki ya kupiga kura na haiwezekani wakaandikishwa kwa muda uliobaki," alisema.
Alisema sababu ya nne ni mashine za BVR kuwa na kasoro nyingi, ikiwamo ya kutotambua alama za vidole gumba vya wananchi ambao wanafanya kazi ngumu, hivyo vidole vyao kuwa na sugu ambao wengi wao ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini.
"Sababu ya tano, ni Nec kupuuza ushauri wa mshauri mwelekezi ambaye aliitahadharisha tume hiyo kwamba haiwezekani kutumia mfumo wa BVR kukamilisha kazi kwa wakati kutokana na changamoto zinazoikabili tume hiyo, ikiwamo ya ukosefu wa fedha, uchache wa watumishi, " alisema.
Akizungumza mapema wiki hii, mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alisema ushauri wa mtaalamu huyo ni wa siku nyingi na kwamba alitaka utumike mfumo wa zamani, lakini tume yake imekataa.
Mchumi huyo, Lipumba alitaja sababu ya sita kuwa ni Nec kutoweza kuandikisha wapigakura wote katika jimbo moja kwa siku saba na kueleza kuwa ni aibu kwa tume hiyo kusema kuwa imeandikisha wapigakura 3,014 katika vituo 55, sawa na wapigakura 54 tu kwa siku kwa kila kituo.
"Sababu ya saba. Ili kuandikisha wananchi milioni 24 wenye haki ya kupiga kura, itahitajika wastani wa siku 55 kila mashine kuandikisha kwenye vituo nchi nzima, tena mashine zisiharibike. Kwa sasa Nec wana mashine 250 tu na nyingine 7,750 hazijulikani zitafika lini," alisema.
Alitaja sababu ya nane kuwa ni Nec kutotoa taarifa za kutosha kwa wadau wote kuhusu teknolojia ya BVR, kutotoa taarifa ya nchi nzima ya vituo vya kuandikishia wapiga kura vilivyopo kila kata, mpaka sasa hakuna mwananchi anayejua.
Profesa Lipumba alisema kama hali ikiendelea hivyo, Ukawa watafungua kesi mahakamani kutaka kusitishwa kwa kura ya maoni kwa sababu Nec haijatoa elimu kwa wananchi, kukiukwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni.
"Taifa litaingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa kama uandikishaji wapigakura hautafanyika kwa ufanisi kabla ya kipindi cha kampeni ya Uchaguzi Mkuu. Tunaitaka Nec ikae na wadau wa Tehama ili kueleza matatizo ya BVR na jinsi ya kutoka hapa tulipo," alisema.
Akizungumzia kuhusu muda mfupi kabla ya tarehe ya Kura ya Maoni mapema wiki hii, Jaji Lubuva alisema wanachoangalia sasa ni kazi ya uandikishaji wapigakura na kwamba kama itashindikana, wataeleza.
Tayari mchakato huo umekumbwa na utata kutokana na wadau kusema kuwa Sheria ya Kura ya Maoni imekiukwa baada ya Rais Kikwete kutangaza tarehe ya kupiga kura. Wanaeleza kuwa Sheria hiyo inaipa Nec mamlaka ya kutangaza siku ya kupiga kura, wakati Rais anatakiwa atangaze kipindi cha Kura ya Maoni.
Mbowe
Akizungumza mashine hizo Mbowe alisema kwa taarifa walizonazo, Makambako kuna mashine 82 na siyo 250 kama Nec inavyodai na kwamba zilizobaki zinatumika kufundishia watumishi wa tume hiyo watakaotumiwa kwenye mikoa mingine."
"Tuna taarifa pia kuwa hawa jamaa wanashinikiza Kura ya Maoni ipigwe Aprili 30 na Katiba ianze kutumika kabla ya Uchaguzi Mkuu, tayari wameanza kubadili baadhi ya sheria."
Mbowe alisema Rais Kikwete asilazimishe kupatikana kwa Katiba mpya ili aondoke katika utawala wake akiiacha nchi ikiwa na amani kama ilivyo sasa.
Kwa upande wake Dk Makaidi alisema tatizo ni Rais Kikwete kutaka Katiba Mpya ipatikane kabla hajaondoka madarakani ilia ache sifa kwa watanzania, jambo ambalo alisema litasababisha machafuko nchini.