Watuhumiwa wanne wa makundi ya uhalifu waliokuwa wamejificha katika mapango ya maji moto eneo la Amboni jijini Tanga, wametiwa mbaroni na jeshi la polisi kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na wananchi wa kata ya Mzizima ambao wameitikia wito wa jeshi hilo ili kuhakikisha wanaishi kwa usalama.
Habari zilizothibitishwa na viongozi wa jeshi la polisi ambao sio wasemaji, baadhi ya watuhumiwa ni wenye asili tofauti wakiwemo wenye asili ya Kiarabu huku wengine wakiwa na asili ya Kisomali ambao wote kwa pamoja wamekamatwa na wananchi kwa kushirikiana na jeshi la polisi hatua iliyosababisha operesheni ya vyombo vya usalama kupunguza kasi tofauti na ilivyokuwa siku nne zilizopita na kusababisha eneo la tukio kuwa kimya kuashiria hali inaelekea kuwa shwari.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo wakielezea jinsi walivyowadhibiti watuhumiwa ambao walikamatwa kwa nyakati tofauti wakiwa wamechoka katika vichaka vilivyopo pembeni mwa mapango ya maji moto yaliyokuwa yakihifadhi wahalifu yaliyopo kilomita 5 kutoka katika yale mapango ya Amboni yaliyozoeleka ambayo yanamilikiwa kisheria na serikali kwa ajili ya kukuza sekta ya utalii, wamesema kukaa na njaa ndio sababu kuu iliyowafanya kuwakamata kiurahisi kisha kuwapigia simu askari wa jeshi la wananchi kwa lengo la kuwakabidhi watuhumiwa.
Hata hivyo jitihada za kumpata kamishna wa operesheni wa jeshi la polisi nchini afande Paul Chagonja ili kutoa taarifa rasmi kuhusu sakata hilo bado zinaendelea lakini awali amekiri kuwa jeshi hilo litawapa motisha watu walioshirikia katika zoezi la kufichua wahalifu hatua ambayo inasubiriwa na wasamaria wema.
via>>ITV