Sunday, February 08, 2015

SERIKALI KUWAPA WAFUNGWA HAKI YA KUPIGA KURA



SERIKALI KUWAPA WAFUNGWA HAKI YA KUPIGA KURA
mhaga
Na Lorietha Laurence-Maelezo,Dodoma
Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wafungwa wote wanaotumikia kifungo chini ya miezi sita na mahabusu wanawapatia haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje aliyehoji kuhusu wafungwa kutoruhusiwa kupiga kura,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Uratibu na Bunge, Jenister Mhagama alisema kwa mujibu wa ibara ya 5(2) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wafungwa wote wenye vifungo chini ya miezi sita wanaruhusia kupiga kura.
Aliongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshaanza kufanya utafiti pamoja na mazungumzo kupitia taasisi mbalimbali zinazohusika na wafungwa kuweka utaratibu wa kuwawezesha kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
'Wafungwa wanaotumikia vifungo vyao chini ya miezi sita wana haki ya kupiga kura ya kuchagua viongozi wao na hiyo imeainishwa katika katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania" alisema Waziri Mhagama.
Aidha aliongeza kuwa kwa wale wanaotumikia vifungo zaidi ya miezi sita Serikali itangalia namna ya kuwasidia kwa kuzingatia sheria na kanuni zinavyosema na kama katiba hairusu basi hawataweza kushiriki kupiga kura.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Maryam Msabaha alihoji kuhusu mpango wa Serikali katika kuwapatia ajira wafungwa walioweza kuhitimu taalum mbalimbali waliokuwa wakitumikia vifungo, ambapo Waziri Mhagama alifafanua kuwa wafuate taratibu na sheria za kuomba ajira.
"Kwa upande wa wale wafungwa wanaohitimu mafunzo mbalimbali yanayotolewa gerezani kabla ya kupata ajira ni vyema wakapata ushauri na baadaye kuajiriwa au kujiajiri wenyewe " alisema Mhagama
Hata hivyo alisisitiza kwamba wafungwa wanapomaliza vifungo vyao huwa watu huru wenye maamuzi yao binafsi katika kuendeleza maisha yao ya kila siku katika kujiletea maendeleo yao.