Kiongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) duniani, Askofu Ted Wilson anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ziara ya kikanisa ya siku nne.
Taarifa iliyotolewa na kanisa hilo, jijini Dar es Salaam, inaonesha kuwa kiongozi huyo anakuja nchini kushiriki Sherehe za Utume zilizoandaliwa na kanisa hilo na kujumuisha nchi zingine 11 za Afrika Mashariki na Kati.
Pamoja na kushiriki kwenye sherehe hizo, lakini kiongozi huyo atashiriki kwenye kuzindua miradi mbalimbali ya afya na elimu ya kanisa hilo nchini.
Sherehe hizo ambazo zinatarajiwa kuvuta zaidi ya watu 50,000 kutoka nchi hizo 11 na sehemu zingine duniani, zitakwenda sambamba na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja kupima afya kwa magonjwa mbalimbali kama ya moyo, sukari, Ukimwi na magonjwa mengine.
Juzi Kiongozi wa Mawasiliano wa kanisa hilo katika ukanda wa Kati na Mashariki mwa Afrika, Mchungaji Steven Bina alisema mkutano huo wa siku nne, ambao unafanyika Uwanja wa Taifa ni wa aina yake na wa kwanza kufanyika nchini.
Katika mfululizo wa sherehe hizo, jana kulizinduliwa ujenzi wa Makao Makuu ya Jimbo la Kusini Mashariki mwa Tanzania (SEC), ambayo yatajengwa katika maeneo ya Kwembe, nje kidogo ya Dar es Salaam.
Shughuli zingine ambazo zilifanyika juzi ni uzinduzi wa kituo cha vitabu, ambacho kipo eneo la Ilala na kitatoa huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambao watahitaji vitabu mbalimbali vikiwemo vya afya na aina vya vyakula vinavyofaa kwa mwili wa binadamu. Kituo hicho kilizinduliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchapishaji ya kanisa hilo duniani, Mchungaji Howard Faigao.
Miongoni mwa shughuli zingine ambazo zitafanywa na kanisa leo ni utoaji wa vitabu 1,000 na jozi 300 za viatu kwa ajili ya shule za msingi, na utoaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari. Vitu hivyo vitatolewa kwa manispaa ya Ilala, ambayo ndio itakayovisambaza mahali ambako kuna mahitaji.
Mkutano huo unahusisha washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eritrea, Somali, Ethiopia, Sudan Kusini na Djibout. Baadhi ya kwaya pia zitatoka nje ya Bara la Afrika.
Tamasha hilo kubwa la kitume, linatarajiwa kuhutubiwa kesho na Rais Jakaya Kikwete. Lakini pia kutakuwepo na viongozi wengine wapatao 400 wa kanisa hilo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Sherehe hizo zenye kauli mbiu ya "Kusherehekea Mibaraka ya Mungu katika Utume", zinafanywa na kanisa hilo ikiwa ni njia ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika upelekaji wa injili na utoaji wa huduma za jamii.