Rais Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, kutokana na vifo vya wanafunzi wawili wa darasa la nne, waliofariki dunia Jumanne wiki hii katika Shule ya Msingi Unity, Mbagala Jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea baada ya gari aina ya RAV 4, kugonga ukuta wa darasa walilokuwemo wanafunzi hao, ambapo wanafunzi wengine watatu walijeruhiwa.
"Nimeshitushwa na kusikitishwa na ajali iliyowatokea wanafunzi hao na kuwapotezea maisha yao wakati wakiendelea na masomo, huku wanafunzi wengine watatu wakijeruhiwa," amesema Rais Kikwete katika salamu zake alizotuma jana kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
"Kutokana na tukio hilo, nakutumia salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kuwapoteza wanafunzi hao, ambao walikuwa tegemeo kubwa kwa Taifa letu," alisema.
Alimuomba Mkuu huyo wa Wilaya, kufikisha salamu hizo za pole kwa wazazi wa wanafunzi hao kwa kupoteza watoto wao, na walimu na wanafunzi wote wa Shule ya Msingi Unity, kwa kuondokewa na wanafunzi hao.
Rais Kikwete amewataka wazazi wa watoto hao wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu mgumu kwao wanapoomboleza msiba wa watoto wao.
"Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza mahala pema peponi roho za marehemu wanafunzi hao," amina.
Aidha, amesema anamuomba Mola awajalie wanafunzi waliojeruhiwa kwenye tukio hilo wapone haraka, ili warejee tena katika hali yao ya kawaida na kuendelea na masomo yao.