Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Salim Shao (kulia) akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 15 Meneja Mkuu wa Kampuni ya Capital Plus International Limited, ambao ni waandaaji wa mbio za Rock City Marathon, Bw. Erasto Kilawe, jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe 15 Novemba mwaka huu.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Salim Shao (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye hafla fupi ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 15 kwa Kampuni ya Capital Plus International Limited, ambao ni waandaaji wa mbio za Rock City Marathon, jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe 15 Novemba. Kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Capital Plus International Limited, Bw. Erasto Kilawe.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Capital Plus International Limited, ambao ni waandaaji wa mbio za Rock City Marathon, Bw. Erasto Kilawe (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye hafla fupi ya kupokea hundi ya shilingi milioni 15 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ikiwa ni udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanzana tarehe 15 Novemba mwaka huu. Kulia ni Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Salim Shao.
NSSF yapiga jeki Rock City Marathon kwa Sh 15M/-
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa shilingi milioni 15 kudhamini mbio za Rock City Marathon mwaka huu, huku waandaaji wa mbio hizo wakitangaza zawadi za washindi.
Jumla ya shilingi milioni kumi zimetengwa kushindaniwa katika makundi mbalimbali ya mbio za mwaka huu zilizopangwa kufanyika Novemba 15 (jumapili hii) katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 15 kwa waratibu wa mbio hizo, Capital Plus International Limited, Afisa uhusiano mwandamizi wa NSSF, Bw. Salim Shao alisema kuwa NSSF imeendelea kudhamini mbio hizo kwa mwaka wa saba mfululizo baada ya kuona maboresho yanayofanyika kila mwaka katika mbio hizo zinazowakutanisha wanariadha kutoka ndani na nje ya nchi.
"Kwa upande wetu tunaona ushiriki wetu katika mbio hizi kama fursa ya kukutana moja kwa moja na wateja wetu lakini pia tutatumia fursa hii kuwaelezea washiriki juu ya umuhimu wa kujiunga na mfuko wetu ili waweze kunufaika na huduma za kipekee zinazotolewa na NSSF," Alisema Bw. Shao.
Mbio za Rock City Marathon, zinazoandaliwa na Kampuni ya Capital Plus International (CPI), kwa ushirikiano na Chama cha Riadha Tanzania (RT), pamoja na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MRAA) zinalenga kutambua na kuinua vipaji vya wanariadha nchini na pia kukuza utalii wa ndani kupitia sekta ya michezo.
Meneja mkuu kutoka kampuni ya Capital Plus International, Bw. Erasto Kilawe, alisema kuwa udhamini huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha hatua za mwisho za maandalizi ya mbio hizo na baadhi ya fedha hizo zitatumika kama zawadi kwa washindi wa mbio za mwaka huu.
"Baada ya kupata udhamini huu, tunafaraja kubwa kutangaza zawadi watakazopatiwa washindi. Kwa mbio za Kilomita 21, jumla ya shilingi milioni saba na laki moja zimetengwa kwa ajili ya washindi. Washindi wa kwanza watazawadiwa Tsh 1.5m/- huku washindi wa pili wakijipatia laki tisa na washindi wa tatu watapata laki saba kila mmoja.
Kwa mbio za kilomita tano, zaidi ya shilingi laki nne zimetengwa kwa ajili ya washindi. Jumla ya shilingi laki tatu na arobaini zimetengwa kwa ajili ya washindi wa mbio za kilomita 3 na shilingi laki mbili imetengwa kama zawadi kwa ajili ya mbio za watoto za kilomita mbili."
Alisema kuwa kamati ya maandalizi ya mbio za mwaka huu imefanya kazi kubwa ili kuhakikisha kuwa kiwango cha mbio hizo kinaongezeka ili kuzifanya ziwe na msisimko zaidi.
"Kwa namna ya kipekee sana nipende kuwashukuru wadhamini wa mbio za mwaka huu ambao ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Precision Air, Bodi ya Utalii Tanzania, New Mwanza Hotel na Bank M," alisema.
Bw. Kilawe alitoa wito kwa wakazi wa jiji la Mwanza na miji jirani kujisajili kwa kuchukua fomu katika uwanja wa Nyamagana.
"Fomu za ushiriki pia zinapatikana katika ofisi za Kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya tatu jengo la ATC, mtaa wa Ohio jijini Dar es salaam na Uwanja wa Amri Abeid mjini Arusha," alihitimisha.