Monday, February 16, 2015

Dawa zilizopigwa ‘stop’ zazagaa mitaani


Dawa zilizopigwa 'stop' zazagaa mitaani


LICHA ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) kufuta usajili na kupiga marufuku uuzaji wa dawa duni, zenye madhara na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu, dawa hizo zimegundulika kuuzwa holela na baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa katika kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza.

Hayo yameelezwa jana na wakazi wa Kisesa wilayani hapa, wakati wa semina ya siku moja iliyojadili visababishi vya ulemavu katika jamii, ambapo walisema madhara ya ulemavu yanatokana na watu kutumia dawa zilizopita muda wake.

Semina hiyo ilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 50 kutoka katika makundi ya walemavu wa kutoona, viungo, kutosikia, uono hafifu, ngozi na watendaji wa vijiji na vitongoji, iliyoandaliwa na asasi ya watu wenye ulemavu ya SANJO na kufadhiliwa na Shirika la the Foundation for Civil Society.

Dawa zilizofutiwa usajili na TFDA ni dawa ya kutibu fungus ( ya vidonge na kapsuli) aina ya Ketoconazole, dawa za kutibu mafua na kikohozi za maji, vidonge na kapsuli zenye kiambato hai aina ya phenylpropanol amine na dawa ya kuua bakteria ya sindano, aina ya Chloramphenicol Sodium Succinate.

Zingine ni dawa ya kuua bakteria ya maji na kapsuli aina ya cloxacillin, malaria ya vidonge yenye mchanganyiko wa Sulphadoxine na Pyrimethamine(SP) na dawa aina ya Amikacin, Levofloxacin.

Watoa huduma pia waliagizwa kusimamia mabadiliko ya matumizi ya dawa aina ya SP ili ziweze kutumika kwa wajawazito tu na dawa aina ya kanamycin, amikacin na Levofloxacin zitumike kwa wagonjwa wa kifua kikuu tu kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Akizungumza katika semina hiyo, mkazi wa Kisesa, Romanus Kalista alisema licha ya Serikali kupitia TFDA kubaini kuwepo kwa dawa duni kwa watumiaji na kufuta usajili wake kwa matumizi ya binadamu, anaona hali hiyo imewachanganya wananchi kutokana na ukweli wananchi wengi kabla ya kufutiwa usajili, walikuwa wakizitumia.

"Hata hivyo dawa hizo zilizopigwa marufuku bado zinatumika hapa Kisesa na TFDA bado haijatoa elimu ya kutosha kwa wananchi, na kibaya ni kwamba dawa hizi bado zinauzwa kwenye maduka ya dawa," alisema. Agnes Mathias ambaye ni mkazi wa Kisesa na ambaye alikiri kuwa aliwahi kufanya kazi ya kuuza dawa katika duka la dawa, aliitaka Serikali itoe elimu zaidi kwa umma.

"Bado dawa zilizopigwa marufuku zinauzwa huku kwetu, mimi nilikuwa muuzaji najua mbinu zinazotumika kuuza dawa, wauzaji wanauza kwa kufungua mlango kidogo, ningeomba serikali ingetuma wataalam waje kufanya ukaguzi vinginevyo madhara yatakuwa makubwa", alionya.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani Iringa, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa, Moses Mbamba alisema wamiliki wa dawa wanaouza dawa hizo zilizofutiwa usajili, wanajali zaidi kutafuta pesa kwa gharama ya maisha ya watu kuliko kujali uhai wa binadamu. Alisema ofisi yake itafanya ukaguzi wa haraka katika eneo hilo.

"Kesho nitamuagiza msaidizi wangu aende huko mara moja kufanya ukaguzi na watakaobainika tutawafikisha mahakamani mara moja, hatutakubali wao kuendelea kuuza dawa zilizofutiwa usajili," aliahidi.