Monday, February 16, 2015

Hali si shwari nchini



Hali si shwari nchini

Dar/Tanga. Ni dhahiri kwamba sasa hali si shwari nchini kutokana na mfululizo wa matukio ya uhalifu ikiwamo kuvamiwa vituo vya polisi, kuuawa kwa polisi na jingine kubwa la juzi la mapigano baina ya polisi wakisaidiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya makundi yanayodhaniwa kuwa ni ya ama ujambazi au kigaidi.

Matukio hayo yanayoliweka Taifa katika wasiwasi zaidi hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamekuwa gumzo kila kona ya nchi kutokana na utata wake.

Katika mfululizo wa matukio hayo, juzi risasi zilirindima mkoani Tanga kwa zaidi ya saa 48 wakati Polisi na askari wa JWTZ waliposhirikiana kupambana na wahalifu hao.

Katika mapambano hayo, askari mmoja wa JWTZ alipoteza maisha na wapiganaji wengine zaidi ya sita kujeruhiwa.

Jana, askari hao waliendelea na operesheni ya kuwasaka watuhumiwa na hadi tunakwenda mitamboni hakukuwa na taarifa zozote za kukamatwa kwao.

Mbali na kutokamatwa watu hao ambao hawajajulikana ni wahalifu wa aina gani, pia silaha zilizokuwa zinasakwa hazikukutwa kwenye Mapango ya Amboni kama ilivyokuwa ikihisiwa, zaidi ya pikipiki moja mbovu na baiskeli tatu. Habari zilizopatikana jana zimedokeza kuwa vikosi vilivyopo katika operesheni hiyo vimebadili mbinu za kuwasaka majambazi hao.

Vilevile, wakazi wa kitongoji cha Karasha Amboni ambao walihama kukimbia mapigano, hadi jana walikuwa hawajarejea majumbani mwao.

Kwa upande wa majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, wanaendelea na matibabu huku madaktari na wauguzi wakitakiwa kutoa taarifa za kila anayefikishwa hapo akiwa majeruhi.

"Tumepewa maelekezo kwamba kila raia anayefikishwa hapa akiwa na majeraha tutoe taarifa haraka kwa uongozi kwani kuna uwezekano wa kuletwa waliofanya mashambulizi kwenye mapango," alisema mmoja wa wauguzi kwa sharti la kutotajwa jina.

Wakazi wa Kijiji cha Kiomoni kilicho jirani na mapango ya Amboni, walisema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikipotosha taarifa juu ya eneo yalikofanyika mapambano, kwamba ni mapango ambayo hutembelewa na watalii na wageni wengine, wakati si kweli.

"Katika eneo la Amboni kuna jumla ya mapango 13 yaliyogunduliwa lakini yanayotumika ni mawili, kwa hiyo kunakoendeshwa mapambano ni pango la mbali kabisa na sehemu inayotembelewa na wageni," alisema Hussein ambaye hufanya kazi ya kupiga picha katika eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai alisema jeshi hilo lisingeweza kuzungumza na vyombo vya habari jana kwa sababu hakukuwa na mtu yeyote aliyekamatwa na operesheni ilikuwa inaendelea. "Sisi sote tuko huku kwenye operesheni na Kamishna (Paul Chagonja wa Operesheni na Mafunzo) hataweza kuzungumza na waandishi wa habari leo (jana) kwa sababu taarifa ni zilezile za jana (juzi)," alisema Kamanda Kashai.

Kaimu Kamanda wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Diwani Athumani alisema matukio ya uhalifu yanayotokea nchini ni mapya na yanayochochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

"Haya ni mambo mapya kwa hapa nchini, lakini ninachoweza kusema ni kuwa, hawa ni wahalifu na ni wachache kiasi kwamba nina uhakika Jeshi la Polisi lina uwezo wa kuwadhibiti," alisema.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mathias Chikawe alisema polisi wanafahamu kuwa kuna hali ya hatari na wameshaongeza ulinzi katika maeneo yote.

"Sisi tunafahamu, ndiyo maana askari wetu tumeshawaambia kuwa sasa hakuna kuning'iniza silaha begani… sasa silaha iwe mkononi wakati wowote kwa mapambano," alisema Waziri Chikawe na kuongeza kuwa juhudi zaidi zinaendelea kufanyika ili kulinda usalama wa raia na kuifanya Tanzania ibaki kuwa kisiwa cha amani.

"Umakini unaendelea, tunahimiza doria na ninakuhakikishia tunapambana nao," alisema Waziri Chikawe huku akisisitiza kuwa ni uhalifu wa kawaida.

Wakati Chikawe akisema hayo, kumekuwapo na taarifa katika vyombo vya habari na wachambuzi wa masuala ya kiusalama zikihusisha uhalifu huo na matukio ya kigaidi yenye lengo la ama kulipiza kisasi cha polisi kupambana na uhalifu au kuteka silaha za kufanyia uhalifu.

Jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alikaririwa akisema mapigano hayo yalifanyika katika msako wa majambazi walioiba silaha kwenye kituo cha polisi mkoani Tanga.

Mwili wa askari wa JWTZ, Said Kajembe aliyefariki dunia katika Hospitali ya Bombo baada ya kujeruhiwa katika mapambano hayo uliagwa jana katika kikosi cha JWTZ Pande na baadaye kusafirishwa kwenda kijijini kwake, Kwashemshi, Korogwe kwa mazishi.

Kaimu DCI Diwani alisema uvamizi huo wakati mwingine husababishwa na wahalifu kutaka kulipiza kisasi kwa polisi hali ambayo alisema inatishia usalama wa nchi kwa ujumla. "Wapo watu wamewekeza kwenye uhalifu, sasa wanapoona polisi wamefanya kazi yao wanaamua kuwaharibia kwa kulipiza kisasi. Kwa kawaida, mhalifu hapendi polisi lakini hawa hawaangalii mbali kuwa vitendo vyao vinaweza kusababisha majanga zaidi ya haya," alisema.

Aliwataka Watanzania kuwa na sauti moja ili kukomesha vitendo vya uhalifu vinavyoendelea nchini ili kuirudisha Tanzania yenye amani.

"Tuwe na sauti moja, wimbo mmoja kama Watanzania, waandishi wa habari ni wadau wakubwa na viongozi wa dini pia watusaidie katika hili. Tunaapa kufanya kazi usiku na mchana kupambana na hili."

Juni mwaka jana, majambazi wanaokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu, walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na kupora bunduki tano na risasi 60.

Polisi aliyeuawa ni Konstebo Joseph Ngonyani na majeruhi Venance Francis na Mariamu Mkamba ambao walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya Mkuranga kwa matibabu.

Septemba mwaka jana, majambazi yalivamia Kituo Kikuu cha Polisi Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na kuua polisi wawili na kujeruhi wengine wawili na kupora bunduki 10 ambazo hata hivyo zilipatikana zote.

Walioawa ni G.2615 PC Dastan Kimati na WP 7106 PC Uria Mwandiga na waliojeruhiwa ni E.5831 CPL David na H627 PC Mohamed. Majambazi hao walivamia kituoni hapo kwa kurusha bomu la mkono.

Januari 15, watu 15 wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za kivita na mabomu ya kurushwa kwa mkono walivamia Kituo cha Polisi Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani na kuua polisi wawili na kupora silaha tano za SMG na mbili za kufyatulia mabomu ya machozi zilizokuwapo kituo hapo na kutokomea kusikojulikana. Katika tukio hilo, polisi wawili Koplo Edga na WP Judith waliuawa.

Februari 3, Kituo cha Polisi cha Mngeta, Wilaya ya Kilombero kilivamiwa na majambazi ambao waliiba bunduki aina ya SMG yenye risasi 30.

Mbali na matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi, kumekuwa na matukio mengine ya uhalifu mkubwa yanayoashiria kuwa hali nchini si shwari, likiwamo la Aprili mwaka jana la majambazi kuvamia Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni, Dar es Salaam na kupora kiasi kikubwa cha fedha.

Katika kipindi hichohicho, majambazi saba wakiwa na silaha waliivamia Benki ya I&M na kupora fedha zinazokadiriwa kuwa ni zaidi ya Sh150 milioni na kutoweka.

Novemba 2013, majambazi wanane walipora zaidi ya Sh900 milioni katika Tawi la Benki ya Habib, Kariakoo, Dar es Salaam. Sh700 milioni na Dola za Marekani 181,885 (Sh285, 444,000).

Mji wa Geita kutekwa kwa dakika 15

Itakumbukwa kuwa Juni mwaka jana, majambazi yaliuteka mji wa Geita kwa takribani dakika 15 na kupora fedha kwenye kampuni ya Blue Coast Inv. na kwa wakala wa usambazaji wa bia wilayani hapo. Kadhalika, majambazi hao walimuua kwa risasi, wakala wa huduma za fedha kwa njia ya simu.

Pia, kumekuwapo na matukio kadhaa ya utekaji mabasi. Januari 20, zaidi ya watu 40 waliteka mabasi sita ya abiria yanayofanya safari kati ya Jiji la Arusha na Nairobi, Kenya.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka aliwataka wananchi kutekeleza majukumu yao badala ya kuwaachia polisi.

"Vyombo vya kisheria na polisi havina watu wa kutosha. Wananchi wanatakiwa kuilinda amani iliyopo. Hili si jukumu la polisi peke yao. Kama tungekuwa na moyo wa kutoa taarifa ya mienendo ya shaka, ingekuwa rahisi kutatua matatizo kwa haraka. Ni muhimu kurudisha ari ya kushirikiana na vyombo vya usalama."

 Mchungaji John Mbata wa Kanisa la Njia ya Yesu, Mbagala alisema hashangazwi na matukio hayo kwani ni dalili ya siku za mwisho... "zamani vituo vya polisi viliogopewa hata kwa kupita tu, leo ndivyo vinavamiwa, hii ni hatari."

Alisema hayo yote ni matokeo ya kumuacha Mungu, hivyo Taifa halina budi kuomba ili uchaguzi ujao uwe na amani.