Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Taifa (Necta) Dk. Charles Msonde.
Hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya waliohusika katika udanganyifu wa mitihani ya kidato cha nne wa mwaka 2014 ambao wanafunzi 184 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu huo.
Kati ya wanafunzi waliofutiwa matokeo 128 ni wa kujitegemea kutoka vituo viwili vya P2617 Kisesa mkoani Mwanza na P4806 Ubago Visiwani Zanzibar na 56 ni watahiniwa kutoka shule mbalimbali.
Akitangaza matokeo juzi jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Taifa (Necta) Dk. Charles Msonde, alisema wameiagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika katika vituo hivyo kwa mujibu wa kanuni za utumishi.
"Lazma wahusika wachukuliwe hatua kwani udanganyifu uliojitokeza ni karatasi moja ya kujibia mtihani kuandikwa na watu watatu tofauti, jambo linaloonyesha hakukuwa na umakini," alisema
Katika matokeo hayo wanafunzi 196,805 (68.33%) wamefaulu kati ya watahiniwa wote 288,247 waliofanya mtihani huo huku kiwango cha ufaulu kikipanda kwa asilimia 10.08 ikilingnishwa wanafunzi 235,22 wailofaulu mwaka 2013 (58.25%).
Hata hivyo, kiwango hicho cha ufaulu bado hakijafikia dhamira ya Serikali ya lengo la Matokeo Makubwa Sasa (BRN) la kufikia aslimia 70, jambo linalohitaji nguvu zaidi kwa walimu, wanafunzi na wadau wote wa elimu.
Dk. Msonde alisema matokeo ya mwaka huu yanaonyesha bado ufaulu wa masomo mengi upo chini ya aslimia 50, Hisabati (19.58), Biashara (34.29), Historia (37.41), Jiografia (37.96), Uraia (37.90), Fizikia (46.71) na Kutunza Fedha (42.20).