KUIBUKA kwa makundi ya vijana ya uhalifu Dar es Salaam, kumesababisha uongozi wa mkoa kuanzisha daftari maalumu la kudumu la taarifa za wahalifu wote wa jiji hilo, ikiwa ni harakati za kumaliza tatizo hilo.
Daftari hilo ambalo litakuwa na kazi ya kutunza orodha ya wahalifu wote kuanzia ngazi za mitaa, litasaidia kuwapata wahalifu kiurahisi watakapofanya matukio katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua mpango wa kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Awamu ya Tatu.
Akifafanua kuhusu kurahisisha kuwapata wahalifu, kutokana na taarifa katika daftari hilo, Sadiki alisema wahalifu watakaorodheshwa katika daftari hilo, kutakuwa na taarifa zao kamili na makosa wanayotuhumiwa nayo, hivyo watakapofanya makosa itajulikana ni akina nani.
"Tunaanzisha benki ya wahalifu ambapo ndani ya daftari hilo kutakuwa na orodha yote ya wahalifu kwa maana hiyo kama mtu kafanya uhalifu eneo fulani, itafuatiliwa kwenye daftari na kujua ni wahalifu gani watakusanya na watakaokuwa hawana hatia wataachiwa," alisema Sadiki.
Alisema katika hilo, hakutakuwa na uonevu wa aina yoyote kwa mtu yeyote, bali watafanya hivyo kwa kufuata haki na sheria. Aidha, alisema madaftari hayo yatakuwepo kuanzia ngazi ya chini ya mitaa hadi ofisi ya mkuu wa mkoa.
"Hapa leo tumezindua mpango mzuri sana, lakini hata tuwe na mipango ya maendeleo mazuri kiasi gani bila kuwa na amani ni sawa na bure, nawaomba chokochoko zozote zinazoweza kuvunja amani tusizifumbie macho," alisema.
Aliwataka madiwani waliohudhuria mkutano huo, kuhakikisha wananchi wao wanaishi kwa usalama na amani kwa kusaidia kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, ikiwemo kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa katika kudhibiti makundi ya uhalifu.
"Kuna makundi ya vijana wahuni kama hawa wanaojiita panya road, mbwa mwitu na mengine ya aina hiyo hawa ni wahalifu, tushirikiane kudhibiti makundi haya kwa kutoa taarifa hata kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na ofisi nyingine za serikali," alisema.
Aidha, Sadiki alionya tabia iliyozuka ya vyama vya siasa kukataa matokeo ya uchaguzi kwa kufanya vurugu. Alisema kufanya hivyo hakuimarishi demokrasia, bali ni kuizorotesha na kuiua.
"Jana tulishuhudia vurugu zilizotokea wakati wenyeviti wa mtaa wa Manispaa ya Kinondoni wakiapishwa, kundi la watu liliibuka na kufanya vurugu, lilijeruhi watu eti wanadai wanapinga wale wanaoapishwa, jamani mbona sheria iko wazi na bahati nzuri kuna watu wanashikiliwa kutokana na tukio hilo," alisema.
Alisema kama watu hao hawakuridhika, walipaswa kufuata taratibu, ikiwemo kwenda mahakamani, lakini demokrasia ya makonde haikubaliki. Alisema amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, kuwachukulia hatua waliofanya tukio hilo bila kujali vyeo au vyama vyao.