Wednesday, December 17, 2014

Washindi bora wa ubunifu wa program za simu wapatikana


Washindi bora wa ubunifu wa program za simu wapatikana
Mshindi wa shindano la kutafuta vipaji vya ugunduzi wa program za simu la AppyStar lililoandaliwa na Vodacom Tanzania Bw.Roman Mbwasi(kushoto)akimsikiliza jambo Meneja wa Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania Abigail Ambweni(kulia)alipotembelea makao makuu ya mtandao huo uliopo Mlimani City jijini Dares Salaam,Mshindi huyu amejinyakulia zawadi ya shilingi milioni 2 na atakwenda Bangalore nchini India kushiriki katika awamu ya pili ya shindano hili ngazi ya kimataifa litakalofanyika Januari 15,2014.
=======  =======  ========
Washindi bora wa ubunifu wa program za simu  wapatikana
v  Ni kupitia shindano la AppStar linaloendeshwa na Vodacom
v  Mshindi wa kwanza kwenda India kushiriki katika ngazi ya kimataifa
Dar es Salaam,December 17,2014: Roman Mbwasi ameibuka mshindi wa kwanza katika shindano la kutafuta vipaji vya ugunduzi wa program za simu la AppyStar lililoandaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom likiwa linawalenga  wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma  masomo ya Sayansi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano na watanzania wote.Wazo la program lililomfanya kuibuka mshindi linahusu upashanaji taarifa za barabarani kupitia mtandao wa simu.

Hii ni mara ya pili kwa Roman Mbwasi kushiriki na kuwa mshindi katika shindano hili mara ya kwanza ikiwa mwaka 2012 ambapo pia aliibuka kuwa mshindi wa kwanza.Kwa ushindi wa mwaka huu amejinyakulia zawadi ya shilingi milioni 2 na atakwenda Bangalore nchini India kushiriki katika awamu ya pili ya shindano hili ngazi ya kimataifa litakalofanyika Januari 15,2014.

Shindano la Appystar lililoandaliwa na Vodacom mbali na kuwalenga wanafunzi wa vyuo ambao walishiriki kwa wingi pia lilikuwa wazi kwa watanzania wote wenye mawazo ya ubunifu wa programu za simu zinazoweza kurahishisha maisha na walitakiwa kuwasilisha  kazi zao kwa kutumia program mbalimbali za kompyuta kama vile   Android, Windows, IOS, na Sumbian.

Nafurahi sana kuibuka tena mshindi  wa mwaka huu na ushindi huu umezidi kunitia moyo katika safari ya kutimiza ndoto yangu ya kuwa mbunifu wa program mbalimbali za kidigitali na nina imani wazo langu lina vigezo vya kushinda katika ngazi ya kimataifa,nashukuru Vodacom kwa kuandaa shindano hili lenye mwelekeo wa  kuibua na kukuza vipaji nchini Tanzania".Alisema Roman

 Washiriki wa mwaka walipangwa katika makundi mawili moja likiwa la wenye makampuni na tayari wana mitandao na wale ambao ndio walikuwa wanaanza kabisa kutangaza ubunifu wao na washiriki  walikuwa wanaruhusiwa kushiriki katika makundi yote mawili.

Washindi wengine ni Athumani Mahiza, George Machibya  na Ilakoze Jumanne .Mshindi wa kwanza kwa kila aina ya kundi lililoshiriki mashindano haya atakwenda nchini India kushiriki mashindano katika ngazi ya kimataifa.

"Mwaka huu mashindano yamezidi kuwa bora na viwango vya  mawazo ya ubunifu yaliyowasilishwa yamekuwa bora zaidi,mfano ni wazo la mshindi wa kwanza Roman ambaye mwaka juzi alishinda kwa wazo la michezo ya kwenye simu mwaka huu ameibuka na wazo la kuboresha taarifa za hali ya barabarani ambalo ni la kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii na hadi sasa program hiyo imeishapakuliwa na watumiaji wa simu zaidi ya 50,000".Anasema Mkuu wa Internet za simu na huduma za ziada wa Vodacom, Saurabh Jaiswal.

Meneja wa Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania Abigail Ambweni anasema:"Ubunifu huu haunufaishi wabunifu wa program bali pia watumiaji wa simu,tukiwa tunaongoza katika  kutoa huduma za mawasiliano kwa njia ya teknolojia,Vodacom ina jukumu la kukuza sekta hii  na kuibua vipaji vya matumizi ya teknolojia ili ziwepo program mbalimbali za kurahisisha maisha kwa watumiaji wa simu".

Washindi wa mwaka huu watapewa zawadi zao Jumamosi ijayo katika hafla itakayofanyika katika ofisi za Vodacom,pia watagharamiwa safari ya kwenda kwenye awamu ya pili ya shindano nchini India ambapo mshindi atakayepatikana atashiriki katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa  wa Masuala ya Simu za mkononi utakaofanyika Barcelona nchini Hispania.

Tangu kuanza mashindano haya mwaka 2012 yametokea kuwavutia washiriki wengi kuutoka nchi mbalimbali.Mwaka huu mashindano haya yamekuwa na washiriki kutoka nchi za , Afrika ya Kusini,,Misri t, Kenya, Ghana na India.